Michezo

Kenya Morans yajiandikia historia mpira wa vikapu Afrika kwa kutinga fainali

July 26th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya mpira wa vikapu ya Kenya almaarufu Morans inazidi kufanya maajabu katika makala ya kwanza ya mashindano ya Bara Afrika (FIBA Afrocan) baada ya kubwaga Morocco kwa alama 96-66 na kuingia fainali Julai 25 jijini Bamako nchini Mali.

Morans, ambayo haijawahi kushinda medali yoyote nje ya mashindano ya Afrika Mashariki katika historia yake, itakutana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika fainali Jumapili.

Dhidi ya Morocco, Kenya ilipata ushindi mkubwa katika robo tatu za kwanza kwa alama 27-11, 23-15 na 27-20. Ingawa ilipoteza robo ya mwisho 19-20, ilikuwa imefanya ya kutosha kujihakikishia itakuwa kwenye jukwaa medali zitakapopeanwa.

Mwanajeshi Erick Mutoro aliongoza ufungaji wa alama za Kenya alipopachika 32 dhidi ya mfungaji bora wa Morocco Sami Al Uariachi (20).

Erick Mutoro akiwa na mpira. Picha/ Hisani

Tangu mashindano haya yaanze Julai 19, Kenya imepoteza mechi moja ambayo ni dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika mechi yyake ya kwanza ya Kundi B.

Kenya, ambayo inaorodheshwa ya chini kabisa katika viwango vya ubora vya mpira wa vikapu katika timu zilizo nchini Mali katika nafasi ya 131 duniani, ililemewa 82-65 dhidi ya DR Congo. Ilipoteza robo zote katika mechi hiyo kwa alama 20-26, 16-17, 12-15 na 17-24 mtawalia.

Kocha Carey Odhiambo wa Morans. Picha/ Hisani

Tylor Okari Ongwae, ambaye anacheza mpira wa vikapu katika klabu ya Bakken Bears Aarhus nchini Denmark, aliongoza ufungaji wa alama za Kenya dhidi ya DR Congo (20), Nigeria (31) na Ivory Coast (24). Griffin Wisyuba Ligare na Tom Bush Wamukota, ambaye ni mwanawe mbunge wa Webuye West, walifungia Kenya alama nyingi dhidi ya Tunisia. Walichangia alama 22 na 21, mtawalia.

Mataifa 12 yalianza mashindano haya na sasa imesalia Kenya na DR Congo kuwania taji.

Timu ya Kenya, ambayo inanolewa na Cliff Owuor na Carey Odhiambo, itakuwa ikitafuta kulipiza kisasi dhidi ya DR Congo katika mechi ambayo bila shaka Morans itahitajika kufanya kazi ya ziada kunyakua medali ya dhahabu.

Kitakuwa kibarua kigumu hasa kwa sababu DR Congo imepiga kila mpinzani imekutana naye ikiwemo miamba Angola 84-78 katika nusu-fainali Alhamisi.

Matokeo ya Kenya Morans:

Julai 19

Kenya 65-82 DR Congo (Kundi B)

Julai 20

Nigeria 69-81 Kenya (Kundi B)

Julai 23

Kenya 85-83 Ivory Coast (Raundi ya 16-bora)

Julai 24

Tunisia 76-82 Kenya (Robo-fainali)

Julai 25

Morocco 66-96 Kenya (Nusu-fainali)

Julai 27

Kenya na DR Congo (Fainali, 9.30pm)

Viwango bora vya dunia vya washiriki:

Nigeria (33), Angola (39), Tunisia (51), Misri (52), Morocco (60), Ivory Coast (64), Mali (68), DR Congo (82), Algeria (95), Chad (99), Guinea (122), Kenya (131).