Kimataifa

Kenya na Mozambique kulegeza kanuni za visa

November 22nd, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Kenya na Mozambique zitaondoa utozwaji ushuru mara mbili na kulegeza kanuni za kupata kibali cha kuingia nchini.

Kulingana na Waziri wa Mashauri ya Kigeni Bi Monicah Juma na mwenzake wa Mozambique Jose Antonio Pachecho, mataifa hayo yameunda kamati ya pamoja kukabiliana na suala hilo.

Hayo yalijiri huku Rais Filipe Nyusi wa Mozambique akitarajiwa kuwasili nchini Kenya Jumatano kwa mkutano rasmi kati yake na Rais Uhuru Kenyatta.

“Makubaliano ya utozaji ushuru mara mbili yanatathminiwa. Yanatarajiwa kukamilika katika muda wa miezi michache ijayo. Tuna matumaini kuwa wakati tutakapofanya mkutano wa pili wa JCC kutakuwa na miradi nyingi itakayokuwa ikiendelea,” alisema.

Biashara kati ya Kenya na Mozambique imeendelea kukua ambapo Kenya imeuzia Mozambique bidhaa za thamani ya dola 11.8 milioni mwaka wa 2017 kutoka $ 6.61 milioni mwaka wa 2006.

Kenya san asana huuzia Mozambique mijengo, bidhaa za plastiki, mafuta kutoka kwa wanyama na mimea, bidhaa za mezani na jikoni, matunda na maji ya mboga miongoni mwa bidhaa zingine.

Kenya huagiza kutoka Mozambique sukari, asali, alumini, makaa, chuma miongoni mwa bidhaa zingine.