Michezo

Kenya na Uganda U-17 waumiza nyasi bure Nairobi

April 2nd, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya soka ya Kenya ya wavulana wasiozidi umri wa miaka 17 imetoka 0-0 dhidi ya majirani Uganda katika mechi ya kujipima nguvu uwanjani Utalii jijini Nairobi mnamo Aprili 2, 2019.

Kenya ilitumia mchuano huu kujipiga msasa kabla ya kuelekea nchini Misri kwa soka ya kimataifa ya Muungano wa Vyama vya Soka vya Kaskazini mwa Afrika (UNAF) yatakayofanyika nchini Misri kati ya Aprili 6 na Aprili 10, 2019.

Akizungumza baada ya matokeo haya, kocha Michael Amenga aliambia Taifa Leo Dijitali kwamba, “Mchuano dhidi ya Uganda ulikuwa mgumu, ambayo ni kitu kizuri kwa sababu mtihani mkali unatusubiri nchini Misri. Sasa nimepata picha kamili ya kikosi changu kitakachosafiri hadi Misri na nimejawa na imani wale nitakaochagua watatumia nafasi hiyo vyema kudhihirisha walistahili kupata namba.”

Timu ya Kenya itaelekea nchini Misri mnamo Aprili 4 kwa mashindano hayo ya mataifa manne yatakayochezwa kwa njia ya mzunguko.

Kenya italimana na Misri, Morocco na Algeria. Uganda ilitumia mchuano dhidi ya Kenya kwa maandalizi ya Kombe la Afrika la Under-17, ambalo Tanzania itaandaa kutoka Aprili 14-28, 2019.