Habari

Kenya nambari tatu ulimwenguni nchi zenye idadi kubwa ya vifaru

January 7th, 2020 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

KENYA imeorodheshwa kama nchi ya tatu ulimwenguni ambayo ina idadi kubwa ya vifaru.

Kulingana na shirika la wanyamapori nchini la KWS, kufikia sasa, Kenya ina zaidi ya vifaru 1,000 idadi ambayo inaifanya Kenya kuwa nchi ya tatu kuwa na idadi hiyo kubwa.

Afrika Kusini na India ndizo nchi za kwanza mtawalia katika idadi kubwa ya vifaru.

Shirika la KWS pia limefichua kuwa Kenya pia ni nambari nne kwa idadi ya ndovu ambao kufikia sasa ni zaidi ya 34,000.

Nchi ya Botswana imesalia kuwa ngome ya ndovu ambao ni zaidi ya 130,000 na ambao hupatikana katika eneo la mito Chobe na Savuti.

Zimbabwe ndio nchi ya pili ikiwa na zaidi ya ndovu 83,000 ambao sana sana wanapatikana katika sehemu za mto Zambezi na mbuga ya wanyama ya Hwange.

Hata hivyo, idadi ya ndovu nchini Zimbabwe imepungua kwa asilimia 10 kutoka mwaka 2005.

Katika taarifa kuhusu hali ya ndovu na vifaru nchini, mkurugenzi wa KWS Brigadier Mstaafu John Waweru alisema kuwa ongezeko la idadi ya wanyama hao linatokana na sheria kali zilizowekwa kuzuia uwindaji haramu.

“Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori na vinginevyo porini na Usimamizi ya mwaka 2013 yaani Wildlife Conservation and Management Act, 2013 ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2019 imesaidia katika kupunguza uwindaji haramu,” akasema Bw Waweru.