Michezo

Kenya nje ya tuzo za wakali wa soka Bara Afrika 2018

December 14th, 2018 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

MATUMAINI ya Kenya kushinda kitu chochote katika Tuzo ya Mwanakandanda Bora wa Afrika mwaka 2018 yameyeyuka baada ya Harambee Stars iliyokuwa imeteuliwa kuwania taji la timu bora ya taifa ya mwaka 2018 kutemwa Ijumaa.

Kocha Mfaransa Sebastien Migne aliongoza Stars kuingia Kombe la Afrika (AFCON) la mwaka 2019 ikimaliza ukame wa miaka 15.

Katika kampeni yake ya kufuzu, Stars, ambayo ilishiriki AFCON mara ya mwisho mwaka 2004, ilishangaza miamba Ghana 1-0 katika mojawapo ya mechi zake za Kundi F, matokeo ambayo Wakenya waliamini yaliifanya kujumuisha na Shirikisho la Soka la Bara Afrika (CAF) katika orodha ya kwanza ya wawaniaji wa tuzo hiyo.

Stars ndiyo ilikuwa inabeba matumaini yote ya Kenya kwa sababu hakuna timu ama mtu mwingine kutoka taifa hili alikuwa ametiwa katika orodha ya wawaniaji. Hata hivyo, Wakenya wengi waliamini Stars haitafika mbali katika tuzo hizi za kila mwaka.

Majirani Uganda wana nafasi nzuri ya kushinda angaa mataji mawili katika hafla ya kutangaza mwanasoka bora itakayofanyika nchini Senegal hapo Januari 7 mwaka 2019. Kenya pamoja Guinea Bissau, Madagascar, Mauritania, Uganda na Zimbabwe zilikuwa zimetiwa katika orodha ya wawaniaji wa taji la timu ya wanaume ya mwaka.

Madagascar na Mauritania, ambazo zimefuzu kushiriki AFCON kwa mara ya kwanza kabisa, pamoja na Uganda iliyojikatia tiketi kushiriki mashindano hayo bila kushindwa, zimesalia mbioni.

Kipa Mganda Denis Onyango, ambaye anasakata soka yake katika klabu ya Mamelodi Sundowns nchini Afrika Kusini, yuko katika orodha ya wawaniaji wa mwanasoka bora wa mwaka wa Bara Afrika. Yeye ni mmoja wa wawaniaji 10 waliosalia mbioni baada ya wawaniaji 24 kuchujwa. Miongoni mwa washindani wakuu wa Onyango ni mabingwa Mohamed Salah wa Misri na Liverpool (2017), Riyad Mahrez kutoka Algeria na Manchester City (2016) na Pierre-Emerick Aubameyang wa Gabon na Arsenal (2015).

Mwanasoka bora wa mwaka wa Afrika (mwanamke) mwaka 2014, 2016 na 2017 Asisast Oshoala kutoka Nigeria yuko katika orodha ya wawaniaji 11 waliosalia mbioni katika kitengo cha wanawake. Mpinzani wake mkuu mwaka 2018 ni Chrestinah Thembi Kgatlana (Afrika Kusini & Houston Dash). Kgatlana ameng’ara sana mwaka huu ikiwemo pia kuibuka mfungaji bora katika Kombe la Afrika (AWCON) lililokamilika nchini Ghana mnamo Desemba 1, 2018.

Orodha ya wawaniaji na vitengo vyao:

Mwanasoka bora wa Afrika mwaka 2018:

 1. Alex Iwobi (Nigeria & Arsenal)
 2. Andre Onana (Cameroon & Ajax)
 3. Anis Badri (Tunisia & Esperance)
 4. Denis Onyango (Uganda & Mamelodi Sundowns)
 5. Mehdi Benatia (Morocco & Juventus)
 6. Mohamed Salah (Misri & Liverpool)
 7. Pierre-Emerick Aubameyang (Gabon & Arsenal)
 8. Riyad Mahrez (Algeria & Manchester City)
 9. Sadio Mane (Senegal & Liverpool)
 10. Walid Soliman (Misri & Ahly)

Mwanasoka bora wa mwaka 2018 (mwanamke):

 1. Abdulai Mukarama (Ghana & Northern Ladies)
 2. Asisat Oshoala (Nigeria & Dilian Quanjian)
 3. Bassira Toure (Mali & AS Mande)
 4. Chrestinah Thembi Kgatlana (Afrika Kusini & Houston Dash)
 5. Elizabeth Addo (Ghana & Seattle Reign)
 6. Francisca Ordega (Nigeria & Washington Spirit)
 7. Gabrielle Aboudi Onguene (Cameroon & CSKA Moscow)
 8. Janine Van Wyk (Afrika Kusini & Houston Dash)
 9. Onome Ebi (Nigeria & Hekan Huisanhang)
 10. Raissa Feudjio (Cameroon & Aland United)
 11. Tabitha Chawinga (Malawi & Jiangsu Suning)

Chipukizi wa mwaka 2018:

 1. Achraf Hakimi (Morocco & Borussia Dortmund)
 2. Franck Kessie (Ivory Coast & AC Milan)
 3. Wilfred Ndidi (Nigeria & Leicester City)

Kocha Bora wa mwaka 2018 (timu ya mwanamume):

 1. Aliou Cisse (Senegal)
 2. Herve Renard (Morocco)
 3. Moine Chaabani (Esperance)

Kocha Bora wa mwaka 2018 (timu ya mwanamume):

 1. Desiree Ellis (Afrika Kusini)
 2. Joseph Brian Ndoko (Cameroon)
 3. Thomas Dennerby (Nigeria)

Timu ya taifa ya wanaume ya mwaka 2018:

 1. Madagascar
 2. Mauritania
 3. Uganda

Timu ya taifa ya wanawake ya mwaka 2018:

 1. Cameroon
 2. Nigeria
 3. Afrika Kusini