Michezo

Kenya hatarini kukosa tena Kombe la Dunia

June 13th, 2024 1 min read

Na CECIL ODONGO

KENYA ina matumaini finyu ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 baada ya kudondosha alama nne katika mechi ya Kundi F dhidi ya Burundi na mabingwa wa Afrika Cote d’Ivoire.

Stars ilicheza mechi hizo jijini Lilongwe, Malawi kwa kuwa nyuga za hapa nchini zinaendelea kufanyiwa ukarabati.

Nyuga hizo ni Nyayo na Kasarani ambazo zinatarajiwa kuwa mwenyeji wa CHAN mnamo Septemba mwaka huu na Kombe la Afrika mnamo 2027.

Vijana wa Kocha Engin Firat walitoka sare ya 1-1 dhidi ya Burundi mnamo Ijumaa wiki jana, kabla ya kutoka sare tasa na Cote d’Ivoire Jumanne.

Baada ya kucheza mechi nne, The Elephants wanaongoza kundi hilo kwa alama 10 huku Gabon ikifuata kwa alama tisa.

Burundi imejizolea alama saba, Kenya alama tano huku Gambia ambao ndio wapinzani wa Kenya katika mechi ijayo, wakiwa na alama tatu. Ushelisheli inavuta mkia kundini bila alama zozote.

Washindi kwenye makundi yote tisa watafuzu Kombe la Dunia moja kwa moja huku timu nne bora katika makundi hayo manne, zikishindana kwenye awamu ya mchujo.

Kuelekea mechi dhidi ya Burundi na Cote d’Ivoire, Kocha Engin Firat alilalamika kuwa kikosi chake kilikuwa na majeraha mengi.

Kati ya wale ambao walisumbuliwa na majeraha ni mabeki Joseph Ouma na Erick Ouma.

Cote d’Ivoire walielekea katika mechi dhidi ya Harambee Stars wakitarajia kuvuna ushindi mkubwa ikizingatiwa Kenya ipo nambari 106 kwa mujibu wa viwango vya soka.

Kilichoponza sana Kenya katika mechi hiyo ni nafasi nyingi za ufungaji wa mabao ambazo waliharibu.

Kenya ilikuwa na nafasi bora ya kufunga bao dakika ya 71 wakati ambapo shuti ya mshambuliaji Michael Olunga iliondolewa kwenye laini ikielekea kujajaa wavuni.

Nao Cote d’Ivoire walipoteza nafasi nzuri zaidi shuti ya Oumar Diakite ikipiga chuma cha goli kabla ya kuondolewa na mabeki wa Harambee Stars.