Habari

Kenya pazuri kupata mkopo mwingine wa Eurobond

March 21st, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

AZMA ya serikali ya kuchukua mkopo wa Eurobond mwaka huu imepigwa jeki kutokana na mazingira ya mikopo yaliyoimarika katika soko la kimataifa.

Hali hiyo imefanya kuwa rahisi kupata mikopo kutoka kwa wakopeshaji wa nje.

Kulingana na Steve Brice, afisa mkuu wa mikakati katika Benki ya Standard Chartered kitengo cha kusimamia mali, viwango vya juu vya riba katika soko la Marekani na dola iliyoimarika vimeendelea kupungua.

Kutokana na hilo, dhamana zinazotolewa na mataifa kama Kenya huvutia bei nzuri.

“Hali hiyo itafanya dhamana ya Kenya kuwa na ushindani sokoni, hivyo bei itavutia zaidi kuliko ilivyokuwa, kwa mfano Septemba mwaka 2018,” alisema Bw Brice.

Kenya inataka mkopo kutoka Eurobond kama moja ya kufadhili upungufu wa bajeti wa Sh635.5 bilioni. Kati ya hizo, Sh321.5 bilioni zinatarajiwa kupatikana kutoka soko la nje.

Hiyo itakuwa ni Eurobond ya tatu baada ya serikali kuchukua Eurobond kwa mara ya pili mwaka jana, ikiwa mpango huo utafanikiwa.

Wakenya watalipa riba ya Sh323 bilioni kutokana na Eurobond ya pili katika muda wa miaka 30 kulingana na Hazina ya Kimataifa ya Fedha (IMF).

Muda wa kuanza kulipa Eurobond 1 umewadia na serikali inatarajiwa kuanza kuzilipa Juni 2019.

Mkopo huo wa Sh280 bilioni uliochukuliwa Juni 2014, na ulikuwa wa kwanza wa aina hiyo kuchukuliwa nchini.