Habari Mseto

Kenya Power kutumia Sh9.5b kuunganisha umeme Nyanza

September 2nd, 2019 1 min read

Na Ruth Mbula

KAMPUNI ya Kenya Power itatumia Sh9.5 bilioni kuunganisha umeme katika eneo la Nyanza Kusini.

Hii ni pamoja na matumizi mengine ya Sh30 milioni ambayo kampuni hiyo inapanga kufungua maeneo ya kitalii.

Maeneo ya Migori, Nyamira, Homabay na Kisii ndio yatakayofaidika kwenye mradi huo ambao unaazimia kuboresha usambazaji wa umeme mashinani na kwenye maeneo ya biashara.

Mradi huo unaunganisha awamu nne zikiwemo uboreshaji wa taa za barabarani, transfoma miongoni mwa miradi mingineyo ya serikali. Akizungumza baada ya mkutano na gavana wa Nyamira John Nyagarama Alhamisi, mkurugenzi wa Kenya Power eneo la Nyanza Kusini Bw John Guda alisema kuwa Sh1.1 bilioni zitatumika katika eneo la Nyamira pekee.

“Tunaazimia kusambaza umeme katika maeneo yote yakiwemo shule za msingi na sekondari, hospitali, viwanda, makanisa na makazi ya wananchi ili kuhakikisha kuwa kila mmoja anapata huduma bora,” akasema.

Gavana Nyangarama alirai kuwa maeneo ya Konate, Nyamira mjini, Kebirigo, Nyaramba, Magombo, Tombe, Makairo, Nyaomite na Kemera yawekwe taa za barabarani haraka iwezekanavyo.

Gavana huyo alisema kuwa kufikia Juni mwaka ujao, matumizi ya nguvu za umeme yataongezeka kutoka asilimia 65 hadi 80.