Habari Mseto

Kenya Power matatani baada ya mama na mwanawe kuuawa na umeme

August 4th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

Kisa cha mama na mwanawe kufariki baada ya kukanyaga waya wa umeme katika kijiji cha Bowa, eneo la Matuga, Kaunti ya Kwale kilichotokea mnamo Julai 31, 2020 ni cha kuhuzunisha na kusikitisha.

Mama huyo mwenye umri wa miaka 34 na mwanawe mchanga, mwenye umri wa miezi mitatu, inasemekana alikuwa akielekea sokoni alipokumbana na mauti.

Kwa mujibu wa picha zilizonaswa, waya huo ulionekana ukining’inia ardhini, licha ya kuwa na nguvu za umeme na kuwa katika njia iliyotumika na wenyeji.

Hata ingawa tukio hilo litachunguzwa na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), Mwakilishi wa wadi eneo hilo, Mwinyi Mwasera alililaumu Shirika la Kusambaza Nguvu za Umeme Nchini – Kenya Power, akisema lilipuuza wito wa wakazi kuwa gogo lililositiri nyaya hizo lilikuwa limeoza.

Isitoshe, inasemekana waya uliosababisha maafa ya mama huyo na mwanawe ulisalia kuanguka kipindi cha wiki mbili zilizopita, jitihada za Mwasera kuwasilisha malalamishi kwa kampuni hiyo zikipuuzwa. Aidha, alisema alijaribu kuwasiliana na maafisa wa Kenya Power eneo hilo kwa njia ya simu bila mafanikio.

“Tunataka Kenya Power iwajibikie tukio hilo, na maafisa hao wahamishwe mara moja,” Bw Mwasera akasema, akitaka familia ya marehemu ifidiwe.

Akithibitisha tukio hilo la kuhuzunisha, Kamanda wa Polisi Kaunti ndogo ya Matuga Bw Joseph Nguli aliwataka wakazi kuwa na subira, huku DCI ikianzisha uchunguzi.

Ikikiri makosa yake, Kenya Power kupitia taarifa kwa vyombo vya habari ilisema uchunguzi zaidi utafanywa na hatua zitakazohitajika kuchukuliwa.

Hata ingawa kifo hakibishi hodi, cha mama huyo na mwanawe kingeepukika iwapo kampuni hiyo ingeitika wito wa wakazi pindi ilipoarifiwa kuanguka kwa waya au nyaya hizo na gogo.

Ni tukio linaloonyesha utepetevu wa Kenya Power, kutowajibika kazini kwa maafisa walioarifiwa na ambao wanapaswa kuchukuliwa hatua kali kisheria, ikiwemo kufutwa na kushtakiwa kortini, badala ya kuhamishiwa sehemu nyingine.

Taasisi nyingi za serikali, maafisa wanapotajwa na umma kutowajibika kazini, hatua inayochukuliwa huwa kuwahamishia eneo lingine. Hiyo ni sawa na kuhamisha taabu, matatizo au mahangaiko kutoka eneo moja hadi lingine.

Si mara moja, mbili au tatu, Shirika la Kenya Power limeenyooshewa kidole cha lawama kwa visa sawa na cha Matuga. Visa vya aina hiyo vimekuwepo, ila havifikii na kuangaziwa na vyombo vya habari.

Ni kufuatia tukio hilo ambapo mwanablogu Coletta Aluda alichapisha kwenye ukurasa wake wa Facebook kikingi cha stima, kinachoelekea kuanguka na nyaya kuning’inia eneo la Kayole, Nairobi.

“Hii ni Matopeni, Kayole, siku 10 baadaye Kenya Power haijafanya lolote (akimaanisha kuchukua hatua). Hatari inayosubiri…” Aluda akaeleza, Pkor Pchirchir Gilbert akichangia na kufichua kuwa aliripoti tukio sawa na hilo na hakuna hatua iliyochukuliwa na kampuni hiyo.

Cliff OJ pia amefichua kwamba kuna gogo la kusitiri nyaya za umeme eneo la Kahawa Wendani, Thika Road, linaloanguka ila shirika hilo halijaitika wito. “Wiki mbili zilizopita, niliripoti kwa Kenya Power gogo linaloanguka Kahawa Wendani. Hakuna hatua iliyochukuliwa kufikia sasa. Gogo hilo linaanguka, nasisitiza njooni muokoe maisha ya watu kabla hasara kutokea,” Cliff akadokeza.

“Inachofanya Kenya Power ni kuongeza bili za stima kiholela. Inapaswa kupelekwa kortini, ishtakiwe na ifidie familia ya mama huyo na mtoto wake,” Shi Norbet akapendekeza.

Baadhi ya wachangiaji pia wanalalamika kampuni hiyo huchukua muda mrefu kurejesha nguvu za umeme zinapopotea, wakiwamulika kwamba wana mazoea ya kufanya kazi usiku na wikendi.

Ni malalamishi kati ya mengi, Wakenya wachangiaji mitandao ya kijamii wakieleza ghadhabu zao.

Kinachojitokeza bayana ni utepetevu katika kampuni hiyo ambayo ndiyo ya kipekee kusambaza nguvu za umeme nchini.