Habari Mseto

Kenya Power yakaidi waziri na kukatia kampuni ya maji umeme

April 7th, 2020 1 min read

Na Waikwa Maina

KAMPUNI ya Umeme ya Kenya (KPLC) Jumatatu ilikatiza huduma za umeme unaosaidia kusambaza maji katika Kaunti ya Nyandarua.

Hii ni kinyume na agizo lililotelewa na Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe ambaye majuma machache yaliyopita aliirai KPLC kutokatiza umeme wakati huu wa kupambana na virusi vya corona.

KPLC ilikatiza huduma za umeme katika visima 15 ambavyo hufikisha maji kwa wakazi 15,000, ikividai deni la Sh1.5 milioni.

Visima hivyo ni Leshao Pondo Kandoro ambacho huhudumia wakazi 2,000 katika eneobunge la Ndaragua, mradi wa maji wa Mugumo katika eneobunge la Ol Kalou na visima vya Weru-Lesirko, Weru-Ex katika eneobunge la Ol Joro Orok. Kisima kingine ni mradi wa maji wa Malewa katika eneobunge la Kipipiri.

Gavana wa Nyandarua Francis Kimemia ameomba KPLC kuhakikisha inarejesha huduma za umeme, akisema wakazi hawafai kukosa maji wakati huu wanapotakiwa kuhakikisha wanadumisha viwango vya juu vya usafi. Alisema serikali yake inalenga kuwalipia wakazi wanaonufaika na maji kutoka visima hivyo deni hilo.

 

Mwakilishi wadi wa Leshao Pondo Kamau Kathangu aliunga kauli ya Bw Kimemia na kuitaka KPLC kurejesha umeme huo haraka iwezekanavyo.