Habari

Kenya Power yalemewa na mzigo wa madeni

November 20th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

CHANGAMOTO zinazoikumba kampuni ya kusambaza umeme nchini Kenya Power, ikiwemo visa vya kupotea kwa stima kila mara, inasababishwa na hali ngumu ya kifedha inayoizonga kutokana na mzigo mkubwa wa madeni, Waziri wa Kawi Charles Keter amefichua.

Bw Keter ambaye alifika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Kawi Alhamisi alisema kampuni hiyo inahitaji usaidizi wa dharura za kifedha akisema imekuwa ikitegemea mikopo kuendesha shughuli zake.

“Tumeanzisha mazungumzo na Hazina ya Kitaifa na wafadhili wengine ili waipige jeki kampuni hii ili kuipunguzia mzigo wa madeni. Mikopo ya kulipwa kwa kipindi kifupi imeongezea Kenya Power masaibu kwa sababu inatozwa riba ya juu. Haiwezi kumudu mikopo aina hii,” waziri Keter akaiambia kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Nyeri Ephraim Maina katika majengo ya bunge, Nairobi.

Aliongeza kuwa Kenya Power inafanya mazungumzo zaidi na taasisi za kifedha za kimataifa kama vile Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika ili zitwae mkopo wake wa kima cha Sh102.6 bilioni na kuipa mkopo utakaolipwa kwa kipindi kirefu.

Mkopo unaolipwa kwa kipindi cha miaka mingi utaipa Kenya Power nafasi ya kulainisha shughuli zake za kuzalisha mapato kwa lengo la kupunguza changamoto za kifedha zinazoizonga.

Kampuni hiyo ambayo ndiyo ina ukiritimba  – monopoly – wa usambazaji umeme nchini imekuwa ikitumia jumla ya Sh25 bilioni kila mwezi kulipia madeni yake.

Maseneta walimsukuma waziri Keter na usimamizi wa Kenya Power kufafanua aina ya mikopo ya kampuni hiyo, huku wengine wakipendekeza kuwa kampuni hiyo inapaswa kuwekwa chini ya usimamizi wa Idara ya Ulinzi kama ya ile ya nyama (KMC).

“Inakera kufahamishwa kwamba kampuni ya kipekee ya kusambaza umeme nchini imelemewa na madeni licha ya kuwatoza wateja ada za juu za kawi hiyo. Hali kama hii haiwezi kukubalika,” akasema Seneta wa Narok Ledama Ole Kina.

Naye Seneta wa Laikipia John Kinyua alipendekeza kuwa kampuni hiyo inafaa kuwekwa chini ya usimamizi wa jeshi kama hatua ya kuiokoa.

Mkurugenzi Mkuu wa Kenya Power Benard Ngugi aliwaambia maseneta hao kwamba madeni mengi ya kampuni hiyo hulipwa kwa safaru ya dola kwa riba ya asilimia 6.5 kila mwaka.

Maseneta walisema riba hiyo ni ghali mno na akatoa wito kwa usimamizi wa Kenya Power kusaka njia za kubadilisha mpango wa ulipaji wa mikopo hiyo.

Kampuni hiyo iliandikisha kupungua kwa faida kwa kima cha asilimia 91.9 hadi Sh262 milini katika mwaka uliokamilika Juni 2020 kutoka faida ya Sh3.3 bilioni wakati kama huo mwaka jana.

Hali hii ilichangiwa na ongezeko la bei ya kununua umeme kwa kima cha Sh18.1 bilioni hadi Sh70.9 bilioni kutoka Sh52.8 bilioni katika kipindi kama hicho mnamo mwaka wa 2018.

Ongezeko la bei ya stima ilipunguza mapato yanayotokana na mauzo ya stima ambayo, hata hivyo, iliongezeka kwa Sh16.9 bilioni hadi Sh112.4 bilioni kutoka Sh95.4 bilioni mwaka uliotangulia, ongezeko la kima cha asilimia 17.8