Habari Mseto

Kenya Power yatahadharisha wakazi kuhusu walaghai

February 17th, 2020 1 min read

Na Mishi Gongo

KAMPUNI ya Kenya Power imeonya kuhusu ongezeko la wizi wa mita pamoja na watu waliowalaghai wakazi Pwani kwa kujifanya maafisa wake.

Kutokana na hali hiyo, wakuu wa kampuni hiyo wamewahimiza wakazi wawe macho na kutoruhusu watu kuangalia mita zao, wahakikishe watu hao wana vitambulisho vya kampuni hiyo.

Meneja wa kampuni hiyo kaunti ya Mombasa, Bw Hick Waswa, alisema wamekuwa wakipokea malalamishi kutoka kwa wakazi ya kuibiwa pesa na watu wanojifanya kuwa mafisa wa Kenya Power.

“Tunahimizi wakazi kabla ya kulipa pesa au kuruhusu mtu kuingia nyumbani kwako,hakikisha ni mfanyikazi wa shirika hili kwa kuangalia kama ana kitambulisho cha kazi,” akasema.

Disemba mwaka jana, wakazi kwenye nyumba 17 wailiandikisha malalamishi kuwa walilaghaiwa na mafisa wa shirika hilo.

Walidai kuwa mafisa hao waliwaagiza kutoa hongo ili wasikatiwe stima.

Hata hivyo Bw Waswa alisema ni hatia kwa afisa wa shirika hilo kuitisha pesa taslim,akisema kuwa malipo yote hufanyika kutumia nambari maalum kupitia simu au benki.

Alisisitiza kuwa maafisa wa shirika hilo hawapokei malipo aina yoyote kupitia pesa taslim.

“Malipo yote yanalipwa kupitia benki au kupitia nambari ya simu,yeyote anaeitisha pesa huyo ni mlaghai na anapaswa kuchukuliwa kama mhalifu,” akasema.

Aidha alidai kuwa afisi inayoshughulikia usalama katika shirika hilo haijapokea taarifa yoyote kutoka kwa walalamishi ambao wanadai kuagizwa kutoa hongo.

Bw Waswa aliwataka wananchi kusoma na kuelewa kipenge katika katiba ya Kinachozungumzia sheria ya nishati ili kuepuka kuvunja sheria.

Kipengee hicho cha mwaka 2019 ni kipya na kinafaa kusomwa.

“Wizi wa stima ni hatia kubwa ambayo inaweza kumpelekea muhisika wa kosa hilo kulipa faini ya hata Sh milioni 10,” akaeleza.

Alisema kumekuwa na visa mbali mbali vya watu kuibiwa mita za stima.

“Wakora wanapoiba mita hizo huishia kuziuza kwa maduka ya vipuri, hii ni hatia kwa kuwa wanaharibia shirika hili jina,” akasema.