Kenya Power yazidi kumulikwa kwa utepetevu

Kenya Power yazidi kumulikwa kwa utepetevu

Na SAMMY WAWERU

KAMPUNI ya usambazaji nguvu za umeme nchini ndiyo Kenya Power inaendelea kumulikwa kutokana na utepetevu wake.

Wakazi wa eneo la Carwash katika mtaa wa Zimmerman, Kaunti ya Nairobi wanalalamikia kuelekea kuanguka kwa kikingi cha kusitiri nyaya za stima.

Vilevile, kikingi hicho kina nyaya zinazoning’inia, hali ambayo inawatia wenyeji wasiwasi kuhusu usalama wao.

Kulingana na wakazi tuliozungumza nao, wanasema kikingi hicho kimesalia katika hali hiyo kwa zaidi ya miezi mitatu.

“Kina zaidi ya miezi mitatu kikiendelea kuinama,” akasema mkazi mmoja, akihofia endapo Kenya Power haitachukua hatua huenda kikasababisha hasara.

Taifa Leo Dijitali ilipozuru eneo ambalo kikingi hicho kinaelekea kuanguka, pembezoni shughuli za kuandaa msingi wa ujenzi wa nyumba zilionekana kutekelezwa.

Isitoshe, kipo barabarani na karibu na majengo ambayo wazingira yake watoto huchezea.

“Ni hatari, hasa kwa watoto wetu ambao huchezea katika mazingira haya,” akateta Daisy Kinyua mkazi, akihoji Kenya Power imearifiwa mara kadhaa ila haijachukua hatua yoyote.

Kinachoshangaza na kuzua hofu zaidi, nyaya zilizopitishwa katika kikingi hicho zinaonekana kuunganishwa kiholela na hafifu.

Visa vya vikingi vya stima kuanguka, nyaya kuning’inia ardhini na pia nguvu za umeme zilizounganishwa kwa njia haramu, vinaendelea kuripotiwa.

Baadhi ya wafanyakazi wa Kenya Power pia wanalaumiwa kufanya kazi kiholela, bila kuzingatia usalama wa mazingira.

Maelfu ya kesi yamerundika kortini, Wakenya wakiishtaki kampuni hiyo kufuatia visa vya watu na mifugo kugongwa na nyaya zenye nguvu za umeme, na kusababisha maafa.

Watu wanaendelea kuhangaishwa na utepetevu wa Kenya Power na uunganishaji wa nyaya isivyofaa, nyaya zenye hitilafu zikitajwa kuongoza kwa visa vya watu wanaoangamizwa na umeme kwa asilimia 24.

Aidha, nyaya zilizounganishwa kwa njia haramu zinawakilisha asilimia 16 ya takwimu za mauaji ya nguvu za umeme, nyumba na majengo yaliyo karibu na vikingi na nyaya za stima asilimia 12 na wanaocheza na umeme kiholela asilimia 9, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa 2020.

Vilevile, takwimu zinaonyesha visa sita vya ajali inayosababishwa na nguvu za umeme Kenya huripotiwa kila mwezi, zaidi ya asilimia 32 ya visa hivyo vikitajwa kushuhudiwa katika makazi ya watu kwa sababu ya nyaya hafifu na mbovu na zilizounganishwa kwa njia haramu.

You can share this post!

Mtihani mgumu unaosubiri Mkenya Onyango kuingiza wanaraga...

Maandalizi ya Idd yanoga Ramadhan ikifika tamati