Habari

Kenya Railways yabomoa majumba ya wafanyabiashara katika kipande chake cha ardhi Nakuru

October 11th, 2020 2 min read

Na MARY WANGARI

MAMIA ya wafanyabiashara katika Kaunti ya Nakuru wanakadiria hasara kuu baada ya Shirika la Reli Nchini (KR) kubomoa majengo yao ya kibiashara usiku wa kuamkia Jumapili, Oktoba 11, 2020.

Shughuli hiyo ya ubomoaji ilifanyika saa kumi alfajiri katika eneo la Barabara ya Geoffrey Kamau, Nakuru, ambapo ilisimamiwa na maafisa wa ulinzi.

Wafanyabiashara wapatao 300 wanaomiliki vilabu, hoteli, vituo vya kuuzia magari na biashara nyinginezo, waliathirika.

Ubomoaji huo unakusudiwa kutoa nafasi kwa ujenzi wa barabara yenye thamani ya Sh160 bilioni kati ya Limuru na Nakuru, kuwa barabara yenye mikondo minne.

Aidha, ubomoaji huo ni sehemu ya maandalizi ya kuifanyia marekebisho reli inayounganisha Nairobi-Nakuru na Kisumu yatakayofanywa na wanajeshi (KDF).

Licha ya KR kueleza kwamba ilikuwa imewapa wafanyabiashara walioathiriwa notisi ya muda wa kutosha wa siku 90, video na picha kupitia vyombo vya habari zilionyesha wapangishaji hao wakifukua vifusi katika juhidi za kuokoa mali yao.

Kulingana na Msimamizi wa Majengo hayo Partrick Nzomo, ubomoaji huo ulitekelezwa ili kuanza mchakato wa kufanyia reli marekebisho.

“Ardhi hii sasa inahitajika kwa lengo la kufanyia reli marekebisho na tayari tumeanza mchakato huo,” alisema Bw Nzomo.

Ardhi hiyo ilikuwa imekodishwa kwa kipindi cha kati ya miaka 15 na 30 ambacho kilikiwa kimekamilika kabla ya KR kuchukua hatua hiyo, kwa mujibu wa ripoti.

Urekebishaji wa reli hiyo unatazamiwa kugharimu kiasi cha Sh3.7 bilioni baada ya miundomsingi hiyo kutekelezwa kwa zaidi ya miaka 25 ambapo shughuli hiyo inatarajiwa kukamilika mnamo Machi 2021.

Baadhi ya wafanyabiashara hata hivyo walifanikiwa kuhamisha mali yao mnamo Jumamosi, Oktoba 10, 2020, huku wakilalamikia kupokea notisi ikiwa imechelewa.

“Mmoja wao alitueleza kwamba tulikuwa na muda wa saa tano kuhamisha mali yetu kutoka majengo hayo na tukikaidi agizo hilo tutajutia sana. Waliweka alama kwenye majengo yatakayobomolewa saa nane,” alisema John Muga, mmiliki wa duka la nguo ambaye ni miongoni mwa wafanyabaishara walioathiriwa,

Ubomoaji huo ni pigo kuu kwa wawekezaji kadhaa waliokuwa wameanzisha biashara zenye thamani ya mamilioni kwenye ardhi hiyo, pasipo kujua kuwa mkataba wa kukodisha ulikuwa umekamilika.