Habari Mseto

Kenya sasa yakopa mabilioni kutoka EU

November 14th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Licha ya kuwa Kenya ina deni kubwa, serikali ilitia sahihi mkopo wa Sh520 bilioni kutoka kwa Muungano wa Ulaya (EU).

Mkopo hu unatarajiwa kulipwa kwa muda wa miaka mitano. Kwa sasa deni nchini ni Sh5.146 trilioni.  Ikilinganishwa na kipindi cha miaka mingine mitano iliyopita ambapo EU ilitoa Sh346 bilioni, mkopo wa sasa umeonekana kuongezwa kwa asilimia kubwa.

Kulingana na EU Jumatatu, mkopo huo ni kuambatana na makubaliano ya ufadhili na ajenda ya serikali.

Makubaliano hayo yalitiwa sahihi na Waziri wa Fedha Henry Roticha na balozi wa EU nchini Stefano Dejak.

Bw Rotich hata hivyo hakueleza ni kiwango kipi kilicho mkopo wa kulipwa na kipi kisicho mkopo wa kulipwa.

EU ilisema pesa hizo zilitolewa kusawazisha wananchi ambao wanatofautiana sana kimapato.

Ufadhili huo unalenga sekta za muundo msingi, uundaji wa nafasi za kazi, kukuza ustahimilivu na usimamizi mwema wa matumizi ya fedha za umma.

Bw Rotich alisema pesa hizo zitatumiwa kukabiliana na changamoto zinazoletwa na mafuriko na ukame.