Michezo

Kenya Shujaa waridhika na nafasi ya 12 Raga ya Dunia baada ya kampeni zilizokuwa zimesalia kufutiliwa mbali

July 1st, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

TIMU ya taifa ya raga ya wanaraga saba kila upande, Shujaa, wamekamilisha kampeni za msimu wa 2019-20 katika nafasi ya 12 kwa alama 35 kwenye msimamo wa jedwali baada ya kunogesha duru sita pekee kati ya 10 za kivumbi hicho.

Hii ni baada ya msimu huu wa vipute vya Raga ya Dunia kwa upande wa wanaume na wanawake kufutiliwa mbali kutokana na janga la corona.

Baada ya kupiga raundi sita, Shujaa waliokuwa chini ya kocha mzawa wa New Zeland, Paul Feeney, waliibuka na ushindi kutokana na mechi saba pekee kati ya 27. Walipoteza mechi 18 na kuambulia sare mara mbili.

Timu za taifa za wanaume na wanawake nchini New Zealand zimetawazwa mabingwa wa Raga ya Dunia muhula huu.

Duru za London, Paris, Singapore na Hong Kong kwa upande wa wanaume zilifutiliwa mbali pamoja na zile za wanawake ambazo zilipangiwa kuchezewa Amerika, Paris na Hong Kong.

“Japo ni masikitiko makubwa kwa wachezaji, mashabiki, waandalizi na kila mhusika, afya ni suala muhimu zaidi. Hili ndilo jambo ambalo jamii nzima ya Raga ya Dunia imelipa kipaumbele,” ikasema sehemu ya taarifa ya Shirikisho la Raga ya Dunia (WR).

“Maamuzi haya ya kufutilia mbali msimu huu ni zao la kushauriana kwa kina kati ya wadau wote na mashirikisho wanachama kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na nchi husika katika juhudi za kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19,” ikaongeza.

Taji la msimu huu kwa kikosi cha New Zealand almaarufu All Blacks ni lao la 13 baada ya kuibuka na ushindi katika raundi tatu kati ya sita zilizokamilishwa kabla ya janga la Covid-19 kubisha na kusababisha kuahirishwa kwa shughuli zote za michezo duniani.

Afrika Kusini waliambulia nafasi ya pili huku mabingwa wa 2019 na mabingwa wa Olimpiki, Fiji wakiridhika na nafasi ya tatu.

Timu ya wanawake ya New Zealand almaarufu Black Ferns walinyanyua ubingwa wao wa pili mfululizo na wa sita chini ya kipindi cha miaka minane.

Kikosi hicho kiliibuka na ushindi katika raundi nne kutokana na tano zilizopigwa kabla ya corona kuvuruga kampeni za msimu huu.

Australia, watakaopania kutetea ubingwa wao wa Olimpiki jijini Tokyo Japan mwaka 2021 waliambulia nafasi ya pili huku Canada wakiridhika na nafasi ya tatu kwa upande wa wanawake.

Kufutiliwa mbali kwa kampeni za msimu huu kunamaanisha kwamba hakuna kikosi kitakachoshushwa ngazi wala kupandishwa daraja baada ya mashindano yote mengine ya mchujo katika madaraja tofauti kutupiliwa mbali.