Michezo

Kenya Simbas kutumia teknolojia ya data kuteua wanaraga wa kushiriki mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia

November 12th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Paul Odera wa timu ya taifa ya wanaraga 15 kila upande, Kenya Simbas, atapania kutegemea huduma za wachezaji bora zaidi katika kampeni zijazo za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia.

Kenya italenga kunogesha fainali hizo zitakazoandaliwa nchini Ufaransa mnamo 2023 kwa mara ya kwanza katika historia.

“Tuna mwaka mmoja pekee wa kujiandaa. Tunalenga kutumia teknolojia ya data kuteua wanaraga mahiri watakaounga kikosi cha kwanza cha Simbas,” akatanguliza.

“Hata mchezaji akiwa Australia, Afrika Kusini, Uingereza, hapa Kenya au popote duniani, tutakuwa na kanzi yao na itakuwa rahisi kufuatilia maendeleo yao na kutathmini ubora wao kabla ya kupata kikosi cha kuwajibisha katika mashindano hayo ya haiba kubwa,” akasema Odera.

“Nakusudia kusuka kikosi chenye mseto wa wachezaji walioanza kucheza raga utotoni na wale waliojitosa katika ulingo huo katika umri mkubwa kidogo. Naamini tutakuwa na kikosi kizuri cha kutisha iwapo tutafaulu kufanikisha hilo,” akaeleza.

Matumaini ya Kenya na vikosi vingine vinavyowania tiketi moja ya ziada ya kunogesha fainali za Kombe la Dunia ni kutwaa kwanza ubingwa wa bara la Afrika mnamo 2022. Afrika Kusini walifuzu moja kwa moja baada ya kutwaa ubingwa wa mwaka jana nchini Japan.

Odera ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20, Chipu, alipokezwa mikoba ya Kenya Simbas mnamo Disemba 2019. Chini ya ukufunzi wake, Chipu waliwahi kunyanyua ubingwa wa Barthes Cup baada ya kuwapiku Namibia mnamo 2019.

Wasaidizi wa Odera katika benchi ya kiufundi ya Simbas kwa sasa ni pamoja na Jimmy Mnene (Meneja wa timu), Ben Mahinda (kocha wa mazoezi), Edwin Boit (mchanganuzi wa kikosi), Michael Owino (kocha wa viungo vya mwili) na Albertus Van Buuren (kocha msaidizi).

Odera ambaye ana cheti cha Raga ya Dunia ya kiwango cha Level 3 katika ukufunzi pia ni mwalimu katika Shule ya Peponi jijini Nairobi.

Simbas walikosa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia zilizoandaliwa nchini Japan mnamo 2019 baada ya kuzidiwa maarifa na Canada, Hong Kong na Ujerumani kwenye mchujo. Nusura wajikatie tiketi ya kunogesha fainali za dunia mnamo 2015 nchini Madagascar ila wakabanduliwa na Zimbabwe kwenye hatua za mwisho za kufuzu.

“Japo Covid-19 imetukosesha fursa ya kushiriki mapambano mengi, kikiwemo kipute cha Africa Cup ambacho tungetumia mwaka huu kujiandalia kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia, bado tuna matumaini tele,” akasema Odera kwa kufichua kwamba wachezaji wake wamekuwa wakijifanyia mazoezi nyumbani katika juhudi za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

“Ilivyo, tutakuwa na msimu mmoja pekee wa 2021-22 kujiandalia kwa fainali za Kombe la Dunia. Huu ni muda mfupi sana kujifua kwa mashindano hayo makubwa. Tumaini la pekee ni kwamba tunajivunia idadi kubwa ya wanaraga bora kimataifa ambao naamini watajituma hata zaidi ya matarajio,” akaongeza.