Michezo

Kenya Simbas yafanya Zambia kitoweo Victoria Cup

July 28th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

TIMU za Kenya na Zimbabwe zimezoa ushindi muhimu ugenini kwenye mechi zao za raga ya wachezaji 15 kila upande ya Victoria Cup, jana Jumamosi.

Hata hivyo, Simbas ilitolewa kijasho katika ushindi wake wa alama 43-23 mjini Kitwe katika mechi ambayo mabingwa hao wa Bara Afrika mwaka 2011 na 2013 waliongoza pembamba 20-13 wakati wa mapumziko.

Mjini Kampala, Zimbabwe pia ilikuwa na kazi nzito dhidi ya Uganda, ambayo ilitoka chini 19-0 na kusawazisha 19-19 kabla ya kupoteza mwelekeo na kupigwa katika ardhi yake 31-26.

Kenya itaalikwa na Zimbabwe katika mechi yake ijayo itakayosakatwa Agosti 3.

Zimbabwe ndio washindi wa Victoria Cup wa mwisho. Walinyakua taji la mwaka 2011 baada ya kuchabanga Wakenya 42-24 jijini Harare na 26-21 jijini Nairobi pamoja na kulima Uganda 25-15 jijini Kampala na 49-21 mjini Bulawayo.

Zambia imejumuishwa katika makala ya mwaka 2019 ambayo ni ya kwanza ya Victoria Cup tangu mwaka 2011.

Ilitoa ushindani mkali kwa Kenya ambayo inaorodheshwa ya 32 duniani. Zambia inashikilia nafasi ya 65 duniani. Zimbabwe na Uganda zinapatikana katika nafasi za 36 na 39, mtawalia.

Mashindano haya yamechukua nafasi ya Kombe la Afrika (Africa Gold Cup) ambayo Shirikisho la Raga la Afrika (CAR) lilifutilia mbali makala ya mwaka 2019 kutokana na ukosefu wa udhamini.

Ratiba ya Victoria Cup (2019)

Julai 13 – Uganda 5-16 Kenya (Elgon Cup & Victoria Cup mjini Kampala), Zimbabwe 39-10 Zambia (Victoria Cup mjini Harare);

Julai 27 – Zambia 23-43 Kenya (Victoria Cup mjini Kitwe), Uganda 26-31 Zimbabwe (Victoria Cup mjini Kampala);

Agosti 3 – Zimbabwe na Kenya (Victoria Cup nchini Zimbabwe);

Agosti 10 – Uganda na Zambia (Victoria Cup mjini Kampala);

Agosti 24 – Kenya na Zambia (Victoria Cup mjini Nairobi);

Septemba 21 – Kenya na Zimbabwe (Victoria Cup mjini Nairobi)