Kenya yaagiza mbegu za GMO

Kenya yaagiza mbegu za GMO

NA LEONARD ONYANGO

WAKULIMA nchini wataanza kupanda mahindi yaliyobadilishwa maumbile kisayansi (GMO) kuanzia mwaka 2023.

Hii ni kufuatia hatua ya serikali kuagiza tani 11 za mbegu za mahindi ya GMO kutoka Afrika Kusini. Mbegu hizo zinatarajiwa kuwasili nchini kati ya Januari na Machi 2023.

Kulingana na Mamlaka ya Kudhibiti Usalama wa Mimea iliyofanyiwa Ukarabati wa Kiteknolojia nchini (NBA), mbegu hizo zinaletwa kufuatia uamuzi wa Baraza la Mawaziri mwezi jana la kuondoa marufuku ya kukuza na kula chakula cha GMO nchini.

Wakati huo huo, NBA imesema haijapokea maombi ya uidhinishaji wa mahindi ya GMO ambayo Waziri wa Biashara, Moses Kuria alisema majuzi kuwa yataingizwa nchini kutoka nje ya nchi.

NBA iliambia Taifa Leo jana Jumanne kuwa mbegu zilizoagizwa kutoka Afrika Kusini, maarufu kama “Bt maize”, haziathiriwi na wadudu ambao huharibu mahindi ya kiasili na tayari zimeidhinishwa kwa mujibu wa sheria.

“Ni mbegu za Bt Maize pekee ambazo zimeidhinishwa humu nchini. Taasisi mbalimbali nchini zimekuwa zikitafiti usalama wa Bt maize na tumeridhika kuwa mahindi hayo ni salama kwa afya na mazingira,” Mkurugenzi Mtendaji wa NBA, Dkt Roy Mugiira aliambia Taifa Leo jana Jumanne.

Dkt Mugiira alisema mahindi hayo ya Bt maize yamekuwa yakifanyiwa utafiti na Shirika la Kutafiti Mazao na Mifugo (Kalro), na kuidhinishwa na Idara ya Kuhakiki Afya ya Mimea (Kephis).

Takwimu za Kalro zinaonyesha kuwa asilimia 12 ya mahindi ya kisasili nchini huharibiwa na wadudu shambani na mbegu za GMO zitamaliza uharibifu huo, kwa mujibu wa NBA.

“Wadudu wanaojulikana kama ‘stem borer’ huharibu mahindi shambani kabla ya mavuno, hivyo kuwaletea wakulima hasara kubwa. Baadhi ya wakulima wamekuwa wakitumia mchanga au majivu kukabiliana na wadudu hao lakini mafanikio ni madogo mno.

“Mahindi ya GMO yataondoa changamoto hiyo inayoletwa na wadudu hao. Mahindi ya GMO huhitaji kunyunyiziwa kemikali ya kuua wadudu mbalimbali wa kuharibu mazao mara tatu tu, tofauti na mahindi ya kiasili ambayo hunyunyiziwa angalau mara 12 hadi kufikia kuvuna,” akasema Dkt Mugiira.

KUHIMILI WADUDU

Akitetea mbegu hizo za GMO, Dkt Mugiira alisema pia haziathiriwi na viwavi wa ‘fall armyworm’ ambao wamekuwa wakihangaisha wakulima kote nchini.

Kenya itakuwa nchi ya nne barani Afrika kuidhinisha mbegu za mahindi hayo ya GMO baada ya Malawi, Nigeria na Afrika Kusini.

Serikali imefichua mipango ya kuleta mbegu hizo siku chache baada ya kutangaza kuwa itaagiza magunia milioni 10 ya mahindi ya GMO kutoka nje ya nchi ili kusaidia mamilioni ya Wakenya wanaohangaishwa na makali ya njaa.

Bw Kuria alisema kuwa atachapisha katika Gazeti Rasmi la Serikali taarifa ya kuruhusu mahindi ya GMO kuingizwa nchini, lakini kufikia sasa hajachapisha taarifa hiyo.

Hatua hiyo ya serikali imekumbwa na upinzani mkali kutoka kwa wanasiasa wakiongozwa na wale kutoka maeneo yanayokuza mahindi, ambao wameitaka serikali kusitisha mpango wa kuleta mahindi ya GMO hadi pale wakulima watakapovuna na kuuza mahindi yao.

Mbunge wa Pokot Kusini, David Pkosing jana Jumanne alitishia kuanzisha mchakato wa kumtimua Bw Kuria iwapo hatafutilia mbali mpango wa kuleta nchini mahindi ya GMO.

Kulingana na Bw Pkosing, shehena hiyo ya mahindi ya GMO itaumiza wakulima katika maeneo ya Bonde la Ufa na Magharibi.

Jana Jumanne, mahindi tani 10,000 yaliwasili katika Bandari ya Mombasa na kuzua uvumi kwamba mahindi ya GMO tayari yameanza kuwasili nchini hata kabla ya kuidhinishwa rasmi na Bw Kuria.

Lakini Taifa Leo baadaye ilibaini kuwa mahindi hayo yalitoka nchini Msumbiji kwa meli ya African Merlin.

“Maafisa wetu walikuwa bandarini na kuthibitisha kuwa mahindi yaliyowasili yalitoka Msumbiji na si ya GMO,” akasema Dkt Mugiira.

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Japan wazamisha chombo cha...

CECIL ODONGO: Ni unafiki viongozi wa Jubilee kumtoroka Raila

T L