Kenya yaamua kusubiri Fifa itoe marufuku ya soka nchini

Kenya yaamua kusubiri Fifa itoe marufuku ya soka nchini

Na JOHN ASHIHUNDU

WAZIRI wa Michezo Amina Mohamed ameanza mazungumzo na Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), lakini amesisitiza kwamba kamati aliyoteua kusimamia shughuli za kandanda nchini itaendelea kutekeleza wajibu wake.

Mkutano wa kwanza kati ya Amina na Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Fatma Samoura ulifanyika Jumatano kupitia mtandao wa Zoom, huku wakitarajiwa kukutana tena juma lijalo.

“Mkutano wetu ulikuwa wa kufana, lakini nilimkumbusha kwamba msimamo wa Serikali kuhusu marufuku ya Shirikisho la Soka Nchini (FKF) hautabadilika. Tutakutana tena wiki ijayo,” aliongeza Amina.

Mnamo Alhamisi Amina alivunjilia mbali FKF na kuteua kamati ya watu 15 kusimamia shughuli za soka kwa miezi sita.

Kamati hiyo ya muda inaongozwa na Jaji Mstaafu Aaron Ringera, huku Fifa ikiionya Kenya kwamba huenda ikachukuliwa hatua kali kwa kuingilia masuala ya mchezo huo.

Mapema juma hili, Fifa ilisema haitatambua kamati hiyo ya muda iliyoundwa, huku ikionya kwamba hatua hiyo ilifanywa kinyume na sheria za Fifa.

Barua ya Fifa ilisema: “FKF inapaswa kuendesha shughuli zao bila kuingiliwa wala kushurutishwa,” barua ya katibu Samoura ilisema.

Chama cha Soka Afrika (CAF) kadhalika kiliteta kuhusu hatua ya Serikali dhidi ya uongozi wa Nick Mwendwa.Kupigwa marufuku kwa FKF kulifuatiwa na kukamatwa kwa Mwendwa ambaye alikuwa ndani kwa siku tatu kabla ya kuachiliwa Jumatatu kwa dhamana.

Tangu achukue usukani, Ringera na kamati yake imesimamisha ligi kubwa za FKF-PL, Supa Ligi (NSL), Ligi Kuu ya Wanawake na ile ya Daraja la Kwanza kwa wiki mbili hadi akutane na viongozi wa timu husika.

Wakati huo huo Korti imempa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji siku saba amfungulia Mwendwa mashtaka ya ubadhirifu wa pesa za umma.

Akitoa uamuzi kuhusu ombi la kuruhusu polisi wamzuilie Mwendwa kwa siku 14 kukamilisha uchunguzi wa ubadhirifu wa Sh38 milioni, Nyamu alisema DPP hakuwasilisha sababu tosha za kumzuilia kinara huyo wa kandanda nchini.

Hakimu alisema endapo DPP hatawasilisha mashtaka dhidi ya Mwendwa faili ya kumchunguza yapasa kufungwa na kumruhusu aendelee na kazi zake.

Nyamu alisema DPP hakuwasilisha cheti cha mashtaka chochote kuonyesha kiasi cha pesa anachodaiwa kutumia vibaya.

Mahakama ilisema polisi itangaza Mwendwa amefuja zaidi ya Sh513 milioni, lakini kortini walisema ni Sh38 milioni zilizotolewa na watu wasioidhinishwa kuendeleza masuala ya kifedha ya FKF.

Kadhalika, alisema polisi walimharibia jina na sifa Mwendwa kwa madai hayo yasiyo na msingi. Mahakama ilisema ilikuwa makosa kwa polisi kumtia nguvuni Mwendwa bila kufanya uchunguzi wa kutosha.

“Polisi walikosea kumzuilia Mwendwa kabla ya kufanya uchunguzi wakutosha,” alisema Nyamu.

Hakimu alisema ni bayana polisi walimshika Mwendwa ndipo watafute ushahidi.Mahakama iliamuru uchunguzi uendelee Mwendwa akiwa nje kwa dhamana ya Sh4 milioni pesa taslimu.

You can share this post!

Wanajeshi waua waandamanaji 14

Kibarua kikali EPL ikirejea

T L