Kenya yaandikisha idadi ya juu zaidi ya maambukizi ya corona tangu Januari

Kenya yaandikisha idadi ya juu zaidi ya maambukizi ya corona tangu Januari

Na CHARLES WASONGA

KENYA iliandikisha idadi ya juu zaidi ya maambukizi ya Covid-19 Jumatano na kuongeza hofu ya wimbi la tatu la maambuzi ya ugonjwa huo hatari.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alitangaza kuwa jumla ya watu 713 walipatana na virusi vya corona baada ya sampuli 5,230 kupimwa ndani ya saa 24 wakati akitoa taarifa hiyo.

Idadi hii ya maambukizi inawakilisha kiwango cha maambukii cha asilimia 13.6 ambacho ni cha juu zaidi tangu Januari.

Akiongea na wanahabari jijini Nairobi baada ya kufanya mkutano na Baraza la Magavana (CoG) waziri Kagwe alitoa wito kwa Wakenya kuendelea kuzingatia masharti ya kuzuia corona kwani “wimbi jipya la maambukizi linaweza kulemea hospitali zetu.”

Bw Kagwe alisema idadi ya wagonjwa wa corona ambao wamelazwa hospitalini pia imeanza kuongezeka tena huku idadi ya wale waliolazwa katika vyumba vya wagonjwa mahututi (ICU) ikifika 89.

“Wakati umefika ambapo tunapaswa kuangalia masharti ambayo tumeweka ili kuona ikiwa tutayaongeza au tutasitisha baadhi. Wakati huu idadi ya maambukizi inaongezeka na kuna hofu kuwa huenda hospitali zetu zikalemewa. Idadi ya wagonjwa katika ICU pia imeenda juu na inakaribia 90,” akasema.

Miongoni mwa wanachama wa CoG waliokuwepo ni mwenyekiti, Martin Nyaga Wambora na Mwenyekiti wa Kamati ya Afya katika Baraza hilo Gavana wa Kisumu Peter Anyang’ Nyong’o.

Wagonjwa wengine 12 pia Jumatano walithibitishwa kufariki kutokana na Covid-19.

Ongezeko la maambukizi limeshuhudiwa siku mbili kabla ya kukamilika kwa kutamatika kwa kipindi cha kafyu ambacho Rais Uhuru Kenyatta aliongeza hadi Machi 12, 2021.

Hali imeibua hofu kwamba huenda Rais Kenyatta aongeza kipindi kingine cha kafyu atakapokuwa akitoa taarifa kuhusu masharti mapya ya kupambana na msambao wa Covid-19 nchini. Kiongozi wa taifa anatarajiwa kutoa taarifa hiyo Ijumaa wiki hii.

You can share this post!

Timu ya tenisi ya meza ya Kenya yaingia Qatar kwa mchujo wa...

Posta Rangers yaipiga Gor Mahia