Michezo

Kenya yaanza Kriketi ya Afrika kwa kuliza Nigeria

May 20th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KENYA imeanza kampeni ya kutafuta mojawapo ya tiketi mbili zilizoko mezani kwenye mashindano ya Kriketi ya Bara Afrika ya kuingia mchujo wa Kombe la Dunia la T20 kwa kucharaza Nigeria kwa wiketi nane jijini Kampala, Uganda, Jumatatu.

Vijana wa kocha Maurice Odumbe walipata alama nyingi za kuzamisha Wanigeria kutoka kwa Dhiren Gondaria na nahodha Shem Ngoche katika uwanja wa Kyambogo.

Jumla ya mataifa sita yanashiriki mchujo huu wa Afrika utakashuhudia mshindi na nambari mbili wakijikatia tiketi ya kushiriki mchujo wa dunia utakaoandaliwa katika Milki za Kiarabu mnamo Oktoba 18 hadi Novemba 15, 2019.

Mataifa mengine yanayowania tiketi hizo mbili ni Uganda, Ghana, Namibia na Botswana. Timu zitakazomaliza mchujo wa Afrika katika nafasi mbili za kwanza zitaungana na Scotland, Zimbabwe, Uholanzi, Hong Kong, Oman na Ireland zilizofuzu kwa kuorodheshwa kutoka nafasi ya 11 hadi 16 duniani kufikia mwisho wa mwaka 2018.

Papua New Guinea ilinyakua tiketi baada ya kushinda mchujo wa East Asia-Pacific mwezi Machi mwaka 2019.

Bara Ulaya na Asia zitachagua wawakilishi wao mwezi Juni na Julai mtawali, huku eneo la Americas ikiandaa mchujo wake mwezi Agosti. Kenya itarejea uwanjani hapo Mei 22 kuvaana na Uganda katika mechi mwanzoni ilikuwa imeratibiwa kuchezwa Mei 19, lakini mvua kubwa ikafanya iahirishwe.

Vikosi:

Kenya – Shem Ngoche (nahodha), Irfan Karim, Alex Auma, Dhiren Gondaria, Rakep Patel, Collins Obuya, Nelson Odhiambo, Sachin Bhudia, Lucas Ndandason, Eugene Odhiambo, Elijah Asoyo, Jasraj Kundi, Pushpak Kerai, Rushabvardhan Patel.