Kimataifa

Kenya yaanza mazungumzo ya kidiplomasia na Tanzania kuzuia uhasama

May 20th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

KENYA imeanza mazungumzo ya kidiplomasia na Tanzania kuzuia uhasama ambao yaelekea umechangiwa na hatua ya Kenya kuamuru kwamba madereva wa matrela kutoka Tanzania sharti wapimwe corona kabla ya kuruhusiwa kuingia nchini.

Hii ni baada ya Tanzania kupiga marafuku magari ya mizigo kutoka Kenya; hatua iliyoonekana kulipiza kisasa hatua hiyo ya Kenya kuweka sharti hilo.

Rais Uhuru Kenyatta pia aliamuru kusitishwa kwa watu kuingia na kutoka Kenya kupitia mpaka baina yake na Tanzania.

Mnamo Jumatatu Kamishna wa Mji wa Tanga Martin Shigela aliamuru kuwa malori ya mizigo kutoka Kenya hayataruhusiwa kuingia Tanzania.

Alisema hayo siku moja baada ya Rais John Pombe Magufuli, mnamo Jumapili, kuhoji hatua ya Kenya kufunga mpaka wake na nchi hiyo.

Ndiposa Jumanne, Balozi wa Kenya nchini Tanzania Dan Kazungu alisema ni kinyume na moyo wa ushirikiano wa kikanda kuzuia malori ya mizigo kutoka Kenya kuingia Tanzania.

Kazungu aliwaambia wanahabari jijini Dar es Salaam kwamba Kenya haijazuia malori ya Tanzania kuingia nchini bali imeamuru kuwa sharti madereva wapimwe corona eneo la mpaka.

Hii ni kulingana na makubaliano kati ya marais ya mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

“Tumelazimika kuchukua hatua kama hii sio kwa lengo la kubagua au kulenga Tanzania, ila lengo letu ni kuzuia kusambaa kwa virusi hatari vya corona. Virusi hivyo ni adui wetu sote. Tukianzisha vita baina yetu, adui huyu ataangamiza idadi kubwa ya watu wetu,” balozi Kazungu akaonya.

Halafu akatoa ufafanuzi.

“Nataka kubainisha kuwa Rais Kenyatta alipotua amri hiyo ya kuzima watu kuingia na kutoka mpaka wa Kenya alisisitiza kuwa magari ya mizigo hayatazuiwa, ila sharti madereva wathibitishwe kuwa hawana Covid-19.”

Kazungu alisema uhasama ulioibuliwa na amri ya Rais Kenyatta unaenda kinyume na malengo ya Jumuiya ya EAC mbayo ni kuhimiza uwiano wa kikanda, upendo, ushirikiano na undugu.

Madereva wa malori kutoka Tanzania wamelalamikia kucheleweshwa kwenye kituo cha mpakani cha Namanga wakisubiri matokeo ya uchunguzi wa Covid-19.

Na akiongea mbele ya kamati ya Seneti kuhusu Ushirikano wa Kikanda Waziri wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Adan Mohammed alisema kuwa Watanzania huenda wakapoteza zaidi katika vuta n’kuvute kati yao na Wakenya.

“Hii ni kwa sababu Tanzania huuza bidhaa nyingi nchini kuliko kiwango cha bidhaa ambazo Kenya huuza huko,” akaambia kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja.

Bw Adan alisema Kenya imejitolea kuhakikisha kuwa usafirishaji wa bidhaa hauathiriwi wakati huu ambapo serikali inatekeleza masharti ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.