Michezo

Kenya yaanza voliboli ya wanaume kwa kutwanga Uganda

June 3rd, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

WENYEJI Kenya wamefaulu kulipiza kisasi dhidi ya Uganda baada ya kutoka seti moja chini na kubwaga 3-2 japo kwa jasho katika mechi yao ya ufunguzi ya michuano ya voliboli ya wanaume ya kufuzu kushiriki mashindano ya Afrika (African Games) katika ukumbi wa kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi, Jumatatu.

Vijana wa kocha Moses Epoloto walitoka chini seti moja na kutwaa ushindi kwa alama 22-25-22, 25-21, 25-21, 25-27 na 15-12.

Mara ya mwisho mataifa haya yalikutana ilikuwa katika mchujo wa kuingia mashindano ya dunia mwaka 2017 nchini Rwanda ambapo Uganda ilikanyaga Kenya kwa seti 3-2.

Washindi wa medali ya shaba mwaka 2011 Kenya walikosa makala yaliyopita ya African Games yaliyopita jijini Brazzaville nchini Congo na wanatamani kurejea katika jukwaa hilo la Afrika mbele ya mashabiki wake uwanjani Kasarani.

Vijana wa kocha Moses Epoloto watavaana na Misri na kisha Rwanda katika mechi zijazo.

Katika mechi ya kufungua mchujo huu wa Ukanda wa Tano uliovutia mataifa manne pekee, mabingwa mara tano wa voliboli ya African Games, Misri walicharaza Rwanda kwa seti 3-1. Mshindi pekee ndiye atajikatia tiketi ya kushiriki makala ya 12 ya mashindano ya African Games yatafanyika nchini Morocco kutoka Agosti 19-31, 2019.

Baada ya siku ya kwanza ya mashindano, Misri inaongoza jedwali kwa alama tatu ikituatiwa na Kenya (mbili), Uganda (moja) nayo Rwanda inavuta mkia bila alama.