Habari

Kenya yaapa kutojadiliana na Al Shabaab

May 21st, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KENYA imesema kamwe haitafanya mazungumzo yoyote na kundi la kigaidi la Al Shabaab ambao waliwateka nyara madaktari wawili kutoka Cuba mjini Mandera mwezi Aprili.

Waziri wa Masuala ya Kigeni Monica Juma Jumanne alisisitiza kuwa Al Shabaab ni kundi la wahalifu na “kisera serikali ya Kenya haiwezi kujadili suala la malipo na watu kama hao,”

Hata hivyo, alisema juhudi zinaendelezwa za kuwakomboa madaktari hao ambao ni miongoni mwa 100 walioletwa nchini kutoa matibabu ya magonjwa sugu katika hospitali za kaunti humu nchini.

“Taifa la Kenya haliwezi kufanya mazungumzo na hata kulipa pesa kwa Al Shabaab ili wawaachilie madaktari hao kwa sababu hili na kundi la wahalifu,” akasema Dkt Juma.

Waziri huyo alisema hayo baada ya kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU) anayesimamia Masuala ya Kigeni na Sera ya Usalama Federica Mogherini.

Dkt Juma alitoa wito kwa EU kusaidia Kenya katika mpango wake wa kutaka Al Shabaab iorodheshwe kama kundi la kigaidi chini ya Mkataba wa Baraza la Umoja wa Mataifa kuhusu Usalama nambari 1267 ya 1999.

Ni mwezi mmoja tangu madaktari hao; Dkt Assel Herera Correa na Dkt Landy Rodriguez watekwe nyara na magaidi wa Al Shabaab mjini Mandera. Katika patashika hilo, mlinzi wao ambaye alikuwa ni polisi wa utawala, alipigwa na kufa.

Majuzi wazee wa jamii ya Kisomali waliotumwa na serikali katika eneo la Jubaland ambako inaaminika madaktari hao wanazuiliwa walisema magaidi hao wanataka walipwe Sh150 milioni ili wawaachilie huru.