Kenya yaendea Morocco fainali ya kufa-kupona kuingia Kombe la Dunia la walemavu

Kenya yaendea Morocco fainali ya kufa-kupona kuingia Kombe la Dunia la walemavu

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA Willis Odhiambo anatumai Kenya itatumia wembe ulionyoa Misri katika nusu-fainali ya kuorodhesha nambari tano hadi nane itakapokutana na Morocco katika fainali ya kufa-kupona ya Kombe la Afrika la soka ya walemavu (CANAF) jijini Dar es Salaam, Tanzania, leo Jumamosi adhuhuri.

Mshindi kati ya Kenya na Morocco ataungana na Ghana, Liberia, Tanzania na Angola katika Kombe la Dunia litakalofanyika Oktoba 2022 nchini Uturuki.

Kenya ilishangaza Misri 5-4 kupitia mabao ya Mohammed Munga (matatu) na Nicholus Keiyo (mawili) nayo Morocco ikalemea Cameroon 4-1 mnamo Alhamisi.

“Ni mechi kawaida kama nyingine, ingawa lazima tumakinike dakika zote 50 kwa sababu hii ni fursa yetu ya pekee ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia. Matumaini yetu ni kuwa kutatandaza kabumbu safi tuliyoonyesha Misri kwa sababu mchezo wao unakaribiana sana,” Odhiambo alisema Ijumaa.

Fainali kuu itakuwa kati ya Ghana na Liberia zilizopiga Angola 3-1 na Tanzania 1-0 katika nusu-fainali mtawalia. Tanzania na mabingwa wa dunia Angola watapepetana kuamua mshindi wa nishani ya shaba. Nambari tano na sita atajulikana kutoka kwa mchuano kati ya Kenya na Morocco.

Misri na Cameroon wanatarajiwa kuwania nambari saba na nane nao Nigeria na Gambia watakabiliana kuamua nafasi ya tisa na 10. Sierra Leone na Zanzibar zitawania nafasi mbili za mwisho.

  • Tags

You can share this post!

Kingi afunguka roho kuhusu PAA, uhusiano wake na Raila

NYOTA WA WIKI: Kylian Mbappe

T L