Makala

Kenya yafaa kujifunza mbinu za kuvuna maji msimu wa mvua

May 15th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

KWA muda wa mwezi mmoja hivi uliopita maeneo mengi nchini yamekuwa yakipokea mvua kubwa.

Hii ni baada ya taifa kukumbwa na ukame, baadhi ya maeneo watu wakiripotiwa kufa njaa.

Hata hivyo, serikali ilikanusha madai ya maafa yatokanayo na njaa ikisema yalitokana na visababishi vinginevyo.

Maeneo yaliyoathirika zaidi ni Marsabit, Wajir, Mandera, Baringo, Turkana, Isiolo, Samburu, Laikipia na Pokot.

Hizi ni miongoni mwa kaunti 13 zilizotajwa, waathirika walipokea chakula cha msaada.

Kiangazi sasa kimesaulika kwa ajili ya mvua inayoendelea kunyea.

Nchini Kenya, ukame umekuwa ratiba ya karibu kila mwaka maeneo yasiyopokea mvua ya kutosha.

Ni kinaya kuona maji ya mvua yanapotea licha ya serikali kudai iko mbioni kuchimba mabwawa – mengi yakitajwa katika sakata za hapa na pale.

Wakati taarifa za ukame kukithiri ziligonga vichwa vya vyombo vya habari, ulikuwa muda mwafaka wa serikali kuu kwa ushirikiano na za kaunti kuangazia suala la upungufu na ukosefu wa maji.

Wachanganuzi wa masuala ya kilimo wanasema njaa ni jambo linaloweza kutatuliwa ikiwa mabwawa ya dharura haswa maeneo kame yatachimbwa.

“Taifa lenye ukwasi wa udongo wenye rutuba kama Kenya halipaswi kulalamika njaa. Mabwawa na hata vidimbwi vikichimbwa wakazi walioko maeneo tata watalima na kupanda mimea kwa ajili ya uzalishaji chakula ama malighafi muhimu.

Njaa itakuwa historia kwao,” anaeleza Bw Meshack Wachira, mtaalamu wa kilimo.

Chini ya katiba inayotumika kwa sasa na iliyozinduliwa 2010, sekta ya kilimo imegatuliwa hivyo basi inaendeshwa na serikali za kaunti.

Kulingana na Bw Wachira, magavana ambao ndio vinara wa kaunti, wanapaswa kuongoza mchakato mzima wa uchimbaji wa viteka maji.

“Wanachohitaji wananchi ni maji wayatumia kuzalisha mazao,” anaendelea kueleza mdau huyu.

Kilimo ni kapu la lishe la taifa hili na ili kuwapa Wakenya motisha kuiboresha, haja ipo kutilia mkazo kuwepo kwa viteka maji.

Mataifa kama Israili na Misri asilimia kubwa huwa ni jangwa lakini njaa ni historia kusikia imewasakama.

Hii ni kwa sababu ipo mikakati ya serikali yza nchi hizo kuvuna maji msimu wa mvua.

Mfano Misri, ni miongoni mwa mzalishaji mkuu wa matufaha.

Israili inajulikana katika kilimo cha maparachichi, ndizi, matufaha, zabibu na stroberi, haya yakiwa machache tu kuorodhesha.

Nchi hizo ‘huvuna’ maji kupitia mabwawa, vidimbwi na matangi msimu wa mvua.

Huyatumia katika kulima, ambapo hutumia mfumo wa mifereji kunyunyizia mashamba maji.

“Maji hayapotei katika mataifa hayo. Yanahakikisha kila tone linatekwa ili kuwafaidi wakulima,” anasema Daniel Mwenda, mtaalamu wa kilimo hasa matunda.

Kulingana na mdau huyu, kwa mujibu wa mvua Kenya hupokea kila mwaka, ni wazi ni nchi inayopaswa kufanya kilimo hadi katika maeneo kame.

Peter Wambugu ni mkulima wa matufaha Laikipia ambayo ni mojawapo ya kaunti kame nchini.

Mwanazaraa huyu amechimba kidimbwi kuvuna maji msimu wa mvua.

Pia, amechimba mashimo yanayochipuka maji kutoka ardhini.

“Hakuna sehemu nchini isiyo na raslimali hii, iwe inayopokea mvua mara kwa mara au kame. Cha muhimu ni kuyateka misimu ya mvua ili yatumike wakati wa kiangazi. Nilipopata kipande cha shamba Laikipia, walionikosoa kuwa nimeenda jangwani sasa ndio wananiiga,” anaeleza Bw Wambugu.

Meneja wake wa matangazo na mauzo Catherine Nyokabi anasema mkondo waliochukua ukifuatwa na wakazi katika kaunti hiyo na zinazodaiwa kame, hadhi yazo itapanda na kuvutia wawekezaji.

“Maeneo yanayosemekana kuwa kame, yanahitaji mwongozo pekee. Ambao utatolewa na serikali ili watu wauige. Kilele chake kitakuwa kutimua njaa,” anasema Bi Nyokabi.

Ni muhimu kukumbusha kuwa maeneo kame nchini pia yana udongo wenye rutuba, hivyo basi ni kiungo tosha cha kufanya kilimo.

Serikali ikitilia mkazo uchimbaji wa mabwawa, vidimbwi, mashimo na hata utumizi wa matenki kuteka maji, miundo msingi kama barabara pia zitaimarika.