Michezo

Kenya yafichua azma ya kuwa mwenyeji wa Diamond League 2023

October 7th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BAADA ya Kenya kuandaa Riadha za Dunia za Mabara za Kip Keino Classic kwa mafanikio makubwa mnamo Oktoba 3, 2020, Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) sasa limefichua mipango ya kuwa mwenyeji wa makala ya mbio za Diamond League mnamo 2023.

Barnaba Korir ambaye alikuwa mkurugenzi wa Kip Keino Classic, amesema kwamba viwango vya maandalizi vilivyoshuhudiwa katika mashindano hayo yalidhihirisha uwezo wa Kenya wa kuandaa mapambano ya haiba kubwa zaidi.

“Mbio za Kip Keino Classic zilitupa jukwaa la kujifundisha mambo mengi ambayo yatatusaidia kuwa wenyeji wa Diamond League baada ya makala mawili yajayo. Lengo letu ni kuleta mashindano hayo hapa Kenya na kudhihirishia ulimwengu ukubwa wa uwezo wetu katika kuandaa matukio makubwa hata zaidi,” akasema Korir.

Tangu yaasisiwe mnamo 2010 kuchukuwa nafasi ya mbio za IAAF Golden League, mashindano ya Diamond League ni miongoni mwa mapambano 15 ya haiba kubwa zaidi ambayo huandaliwa na Shirikisho la Riadha Duniani (WA) kila mwaka.

Mbio hizo hujumuisha fani 16 tofauti zikiwemo mbio za mita 100, mita 200, mita 400, mita 400 kuruka viunzi, mita 800, urushaji wa kijiwe, urushaji wa kisahani, urushaji wa mkuki, kuruka juu na kuruka juu kwa upande wa wanawake na wanaume.

Hadi kufikia sasa, ni jiji la Rabat, Morocco ndilo la pekee barani Afrika linalojivunia tija na fahari ya kuwahi kuandaa mbio za Diamond League mnamo Mei 2016.

Riadha za Dunia za Mabara almaarufu World Continental Tour ndiyo ya pili baada ya Diamond League inayofuata Riadha za Dunia (World Athletics Championships) kwenye orodha ya mashindano ya haiba kubwa zaidi kwenye ulingo wa mbio duniani.

Korir amefichua kwamba Kamati Andalizi ya Kip Keino Classic sasa itatalii baadhi ya mapungufu machache yaliyoshuhudiwa kwenye mbio hizo za Oktoba 3 kabla ya kubuni mikakati maridhawa zaidi itakayofanikisha maandalizi ya Diamond League mnamo 2023.

Riadha za Kip Keino Classic ndiyo mashindano ya kwanza ya haiba kubwa kuwahi kufanyika barani Afrika tangu kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19 uliositisha shughuli nyingi za michezo duniani kote kuanzia Machi mwaka huu.

“Haimaanishi kwamba tutaridhika na ufanisi tulioshuhudia ugani Nyayo wakati wa kuandaliwa kwa mbio za Kip Keino. AK itazidi kushirikiana na Wizara ya Michezo kutalii uwezekano wa kupanua zaidi miundo-misingi iliyopo na kuwapa wanariadha wetu vifaa na mazingira mwafaka zaidi ya kujikuza kitaaluma,” akaongeza kinara huyo.

Licha ya changamoto tele za kifedha zilizochangiwa na janga la corona, Wakenya walitia fora katika mbio za Kip Keino Classic ambazo zilihudhuriwa na mashabiki 6,000. Mbio hizo zilivutia zaidi ya wanariadha 150 kutoka mataifa 30 tofauti.

Kati ya Wakenya waliotamba katika mbio hizo ni mabingwa wa dunia Hellen Obiri, Timothy Cheruiyot na Beatrice Chepkoech waliotawala vitengo vyao vya mita 5,000, mita 1,500 na mita 3,000 kuruka viunzi na vidimbwi vya maji mtawalia.