Habari

Kenya yafungia nje Amerika, TZ

July 31st, 2020 2 min read

Na VALENTINE OBARA

SERIKALI imeamua kuruhusu raia wa kigeni kutoka mataifa 11 pekee kuingia nchini wakati safari za ndege za kimataifa zitakaproanza tena kesho, huku Tanzania na Amerika zikiwa kati ya nchi zilizofungiwa nje.

Safari za ndege za kimataifa zilikuwa zimepigwa marufuku Machi wakati maambukizi ya virusi vya corona yalianza kushuhudiwa nchini.

Waziri wa Uchukuzi, Bw James Macharia, Alhamisi alitangaza kuwa Kenya itaruhusu wageni kutoka China, Korea Kusini, Japan, Canada, Zimbabwe, Ethiopia, Uswisi, Rwanda, Uganda, Namibia na Morocco.

Alieleza kuwa, uamuzi huo umechukuliwa kwa kuzingatia kiwango cha maambukizi ya Covid-19 katika kila nchi.

“Hizi ndizo nchi zilizo na idadi ndogo ya maambukizi, maambukizi ambayo hayana madhara sana ama idadi ya maambukizi yapungua kwa kasi katika nchi hizo,” akasema waziri.

Hali ya virusi vya corona Tanzania haijulikani kwa vile serikali ya Rais John Pombe Magufuli iliacha kutoa matangazo ingawa serikali hiyo husema imefanikiwa kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo hatarii.

Kwa upande mwingine, Amerika yaongoza kwa idadi ya maambukizi ulimwenguni ambapo jana kulikuwa na visa 4,583,662 vya maambukizi, na vifo 154,187.

Orodha ya mataifa yatakayoruhusiwa kuingia nchini ilikosa pia kujumuisha nchi za Ulaya ambapo maambukizi yanaenea kwa kasi, mataifa mengi ya Asia, Uingereza na Afrika Kusini ambayo ndiyo inaongoza kwa idadi ya maambukizi Afrika.

Wasafiri wanaoingia nchini watahitajika kuwa na cheti cha kuthibitisha hawajaambukizwa virusi vya corona.

Cheti hicho kitahitajika kuonyesha kuwa msafiri alipimwa siku nne kabla ya safari yake.

Bw Macharia alithibitisha kuwa wasafiri watakaowasili nchini bila dalili za corona hawatahitajika kwenda karantini.

Kwa wasafiri wanaoenda nje ya nchi, serikali imesema itawahitaji kufuata kanuni zote za nchi ambako wanaelekea.

Waziri huyo alieleza kuwa maamuzi haya yamechukuliwa kwa lengo la kuinua uchumi.

Hayo yalijiri wakati idadi ya maambukizi inaendelea kuongezeka nchini.

Jana, visa vipya vya maambukizi 788 vilitangazwa na kufikisha idadi ya jumla kuwa 19,913. Wagonjwa 100 walithibitishwa kupona na kufikisha idadi ya jumla kuwa 8,121.

Katika hotuba yake, Waziri Msaidizi wa Afya, Dkt Rashid Aman, alisema wagonjwa 14 walifariki na hivyo kufikisha idadi hiyo kuwa 235.

Kaimu Mkurugenzi wa Afya ya Umma, Dkt Patrick Amoth, alisema kuna wagonjwa 1,275 ambao wamelazwa hospitalini, na 56 kati yao wako katika vyumba vya wagonjwa mahututi.

Alifichua kuwa miongoni mwa waliofariki jana, tisa hawakuwa na magonjwa mengine isipokuwa Covid-19.

“Wengi wanaofariki bila magonjwa mengine ni vijana ndiposa tunawasihi vijana kuchukulia ugonjwa huu kwa uzito,” akasema.

Kwingineko, mtaalamu wa magonjwa ya kuambukizana, Dkt Anthony Fauci, amependekeza watu waanze kuziba macho yao sawa na wafanyavyo pua na midomo wanapovalia barakoa.

Kulingana na daktari huyo ambaye anategemewa sana Amerika katika vita dhidi ya virusi vya corona, ni hatua ya busara mtu yeyote aliye na vifaa vya kufunika macho kama vile miwani mikubwa almaarufu ‘goggles’ wavitumie hasa wakiwa maeneo ya hadhara.

Alitoa ushauri huo alipohojiwa na shirika la habari la ABC, wakati ushahidi umeonyesha viini vya corona huweza kuelea hewani kwa muda.

“Binadamu wana utando telezi ndani ya pua, midomo na pia machoni. Kimsingi, unapaswa kuziba sehemu hizo zote. Kwa hivyo kama una vifaa vya kuziba uchafu kuingia machoni, vitumie,” akasema.

Alifafanua kwamba ingawa ushauri huo haujapitishwa kimataifa kwa sasa, ni vyema kufuatwa na mtu yeyote ambaye anataka kujilinda kikamilifu dhidi ya ugonjwa wa Covid-19.