Habari za Kitaifa

Kenya yageukia tena China kwa mikopo


KENYA imegeukia China kuisaidia kupata ufadhili wa miradi ya maendeleo, miaka miwili baada ya Serikali ya Kenya Kwanza kukumbatia Amerika na mataifa ya Ulaya kama washirika wake wakuu.

Baada ya kuingia mamlakani, serikali ya Kenya Kwanza chini ya uongozi wa Rais William Ruto, ilionekana kuchangamkia Amerika na mataifa ya Magharibi huku uhusiano wake na China ukionekana kuingia baridi.

Mnamo Jumatatu, Septemba 2, 2024, Rais William Ruto alianza ziara yake China kuhudhuria kongamano la ushirikiano wa Afrika na China huku nchi hiyo yenye uwezo mkubwa Bara Asia ikilegeza masharti yake ya mikopo kwa bara la Afrika.

Katika ziara hiyo, Rais Ruto aliweka msingi wa ufufuzi wa uhusiano wa Kenya na China ambao uliwezesha ujenzi wa miundomsingi muhimu nchini ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR) na barabara ya Nairobi Expressway miongoni mwa mingine.

Jumanne, Septemba 3, 2024, Rais Ruto na ujumbe wake walikutana na Rais wa China Xi Jinping katika mazungumzo ya nchi hizi mbili ambapo alifungua soko la bidhaa za kilimo kutoka Kenya katika nchi hiyo ya Asia.

“Nilifanya mazungumzo na Rais Xi Jinping jijini Beijing, China, kabla ya kongamano la ushirikiano wa Afrika na China. Katika mkutano huo, Rais Xi alikubali mazao ya kilimo kutoka Kenya kuuzwa katika soko la China,” Rais Ruto alitangaza kupitia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii.

Katika hali iliyoonekana kama ufanisi wa mazungumzo hayo, Rais Ruto alisema walikubaliana kujadili miradi ya maendeleo kama vile upanuzi wa SGR na barabara kuu ya Rironi-Mau Summit hadi Malaba.

Licha ya kuonekana kuegemea mataifa ya Ulaya na Amerika ambayo amezuru mara kadhaa ikiwemo mwaliko katika Ikulu ya White House ambako utawala wa Rais Joe Biden ulitangaza uwekezaji wa mabilioni ya pesa nchini, Rais Ruto alisisitiza kuwa uhusiano wa Kenya na China haujayumba. “Kenya na China zina uhusiano mzuri wa kidiplomasia. Uhusiano huu umekuwa na manufaa ya kirafiki kwa nchi zetu mbili na kubadilisha pakubwa miundomsingi ya reli, barabara na bandari za Kenya,” Rais Ruto alisema.

Kenya imeonekana kugeukia China wakati nchi hiyo imepunguza mikopo na kuacha kufadhili miradi kama barabara, bandari na reli.

Kenya ambayo imekuwa ikinufaika na mikopo kutoka China ilipata mkopo wa mwisho kutoka kwa nchi hiyo 2019, kulingana na utafiti wa kituo cha Kimataifa cha Maendeleo ya Sera cha Chuo Kikuu cha Boston ambacho kina mradi unaofuatilia mikopo ambayo China inayapa mataifa ya Afrika.

Ripoti hiyo inasema Kenya na Ethiopia ni miongoni mwa mataifa ya Afrika yaliyopata mikopo mingi kutoka China ambayo hayakupata mikopo mipya kutokana na au baada ya janga la Covid-19.

Kutokana na hatua hii, Misri iliongoza kwa mikopo kutoka China na kushikilia nafasi ya tatu kutoka ya tano 2019.

Rais Ruto alitarajiwa kujadili mikopo ya kupanua SGR kutoka Suswa karibu na Naivasha hadi Kisumu na Malaba, ujenzi wa barabara za maeneo ya mashambani Kenya na mfumo wa uchukuzi wa kisasa katika Kaunti ya Nairobi.

Katika ziara yake Amerika mnamo Mei 2024, Dkt Ruto alivunia Kenya uwekezaji na ufadhili wa mabilioni ya pesa kupitia mipango na miradi mbalimbali.

Mipango hiyo inahusiana na ukuzaji wa demokrasia, haki za binadamu na utawala, ushirikiano katika sekta ya afya, kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, biashara na uwekezaji, teknolojia ya dijitali, amani na usalama.

Rais Ruto pia alipata ufadhili wa Sh477 bilioni kujenga Barabara Kuu ya Nairobi hadi Mombasa kuwa ya laini nne kila upande miongoni mwa miradi mingine.

Kampuni kubwa za teknolojia zenye makao makuu Amerika pia zinatarajiwa kuwekeza Kenya na kuunda nafasi za kazi.