Kenya yahimizwa kuchukua bima dhidi ya majanga

Kenya yahimizwa kuchukua bima dhidi ya majanga

NA MARY WANGARI

KENYA ni miongoni mwa mataifa ya Afrika ambayo yamehimizwa kuanza kutumia mbinu za kisasa kama vile bima kufidia waathiriwa wa majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Kinyume na kutegemea mbinu za kijadi kupitia msaada kutoka kwa wahisani, serikali ya Kenya imeshauriwa kuchukua bima katika viwango vya kitaifa na kaunti dhidi ya majanga kama vile mafuriko na kiangazi yanayozidi kuongezeka.

“Tunaamini kuwa bima ni bora zaidi kushinda mbinu za kijadi za kutegemea msaada wa kibinadamu ambao unaweza kuchukua hadi muda wa miezi tisa kukusanya na kusambazia watu,” alisema Mkurugenzi wa Shirika kuhusu Majanga Afrika (ARC) Lesley Ndlovu.

Akihutubia vyombo vya habari jana Alhamisi jijini Nairobi, Bw Ndlovu alisema, “Mpango wa bima kwa kawaida hutoa malipo katika muda wa siku 4-10, unaopatia serikali ufadhili wa kwanza unaohitajika ili kuchukua hatua thabiti.”

Kenya ni moja kati ya mataifa 55 barani Afrika yaliyoasisi na kutia saini Mkataba wa ARC ambapo ilichukua bima kwa mwaka au msimu mmoja pekee 2013-2017 kabla ya kuacha.

Kwa sasa, shirika hilo linatoa bima kwa watu 30 milioni Afrika dhidi ya ukame, mafuriko na vimbunga huku idadi ya watu wanaohitaji bima hiyo Afrika ikifikia 700 milioni.

“Kinachotukosesha usingizi usiku ni kusaka mbinu za kibunifu za kupanua vitengo za bima zetu ili kufadhili bara zima kwa sababu tunaamini bima ni muhimu kwa kuwezesha fedha kupatikana na watu wanaozihitaji kwa wakati ufaao na kwa namna inayofaa,” alisema Bw Ndlovu.

Hazina ya Kinga Dhidi ya Majanga kutokana na Mabadiliko ya Tabianchi Duniani iliyozunduliwa majuzi katika Kongamano Kuu la COP27 ilifungua njia kwa mataifa yanayoendelea Afrika kupata ufadhili wa kifedha kufuatia majanga.

  • Tags

You can share this post!

Muuzaji nyama atozwa faini ya Sh1,000 au jela siku 14 kwa...

Kiungo Mkenya ajiunga na klabu ya amputee nchini Uturuki

T L