Michezo

Kenya yaifundisha Rwanda voliboli

May 19th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MALKIA Strikers ya Kenya imeanza kampeni zake za kufuzu kwa mashindano ya voliboli ya All-African kwa kishindo baada ya kuchabanga Rwanda kwa seti 3-0 jijini Kampala nchini Uganda, Jumapili.

Ikianzisha wachezaji wake wakali zaidi Mercy Mim, Noel Murambi, Violet Makuto, Jane Wacu, Edith Wisa, Trizah Atuka na Agrippina Kundu, Kenya ilishinda seti hizo kwa alama 25-10, 25-17 na 25-10.

Rwanda ilidhaniwa itababaisha Kenya katika mashindano haya, lakini inavyoonekana mabingwa mara nne wa All-African Games, Kenya watakuwa na mtihani rahisi kuelekea Morocco kwa makala ya mwaka huu yatakayofanyika mjini Rabat mwezi Agosti.

Kabla ya kunyakua tiketi hata hivyo, Kenya italimana na Ethiopia hapo Mei 20 na kufunga kazi mnamo Mei 21 dhidi ya wenyeji Uganda.

Mshindi wa mashindano haya ya Ukanda wa Tano yaliyovutia mataifa manne pekee baada ya Misri kujiondoa dakika ya mwisho ataingia mashindano ya Bara Afrika ya All-African.

Ratiba: Mei 20 – Ethiopia na Kenya (6.00pm), Uganda na Rwanda (8.00pm); Mei 21 – Rwanda na Ethiopia (6.00pm), Kenya na Uganda (8.00pm).