Michezo

Kenya yaikaba Cote d’Ivoire mechi ya kufuzu Kombe la Dunia

June 11th, 2024 2 min read

Na CECIL ODONGO

HARAMBEE Stars Jumanne ilicheza kibabe na kuwakaba mabingwa wa Afrika Cote d’Ivoire kwa sare tasa katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 nchini Malawi.

Mtanange huo wa kundi F uligaragazwa katika uwanja wa kitaifa wa Bingu, jijini Lilongwe. Hii ilikuwa mara ya kwanza Kenya ilikuwa ikichuana na Cote d’Ivoire katika soka.

Ilichezwa wakati ambapo taifa hilo linaendelea kuomboleza mauti ya Makamu wa Rais Dkt Saulos Chilima na watu wengine saba ambao waliaga kwenye ajali ya ndege  katika milima ya Chikangwa mnamo Jumatatu.

Kenya ilielekea katika mchuano huo baada ya kuagana sare ya 1-1 na Burundi mnamo Ijumaa wiki jana. Kwa upande mwingine, Cote d’Ivoire ilikuwa imepiga Gabon 1-0 Jumamosi iliyopita.

Sare hiyo inaicha Kenya ikiwa kwenye nafasi ya tatu kwenye kundi F kwa alama tano huku Cote d’Ivoire ikiongoza kundi hilo kwa alama 10. Gabon ambayo ilitarajiwa kucheza na Gambia baadaye Jumanne ina alama sita.

Gambia imejizolea alama tatu nayo Ushelisheli inakokota nanga bila alama zozote na ilitarajiwa kuchuana na Burundi kuanzia saa nne usiku wa Jumanne.

Kabla ya mechi hiyo kuliibuka tetesi kuwa kambi ya Stars iligubikwa na uhasama wa ndani kwa ndani na wachezaji walikuwa wametishia kususia kabiliano ya Cote d’Ivoire.

Kocha Engin Firat alifanya badiliko moja pekee katika kikosi kilichocheza dhidi ya Burundi ambapo alimwaanzisha beki Alphonce Omija kwenye nafasi ya winga wa AFC Leopards Clifton Miheso.

Cote d’Ivoire ambayo ilitwaa ubingwa wa Afrika mnamo Januari 2024  nchini mwao nao walimkosa nyota wa Borussia Dortmund Sebastian Haller anayeuguza jeraha.

Katika kipindi cha kwanza, Stars ilipata nafasi kadhaa za wazi za kufunga lakini ikashindwa kuzitumia. Dakika ya 28, nahodha Michael Olunga alichanja mpira wa ikabu kwa ustadi mkubwa lakini ukaishia mkononi mwa mnyakaji Yahia Fofana.

Cote d’Ivoire maarufu kama The Elephants nao walilia chooni baada ya kiungo Seko Fofana kuachilia fataki iliyoishia nje mita chache kutoka kwa goli la Stars, kipa Patrick Matasi akiwa amesimama upande mwingine wa goli.

Katika kipindi cha pili, Star walipoteza nafasi mbili, moja Olunga akiachilia shutu lakini Ghislain Konan akauzuia kisha Richard Odada akauwahi lakini ukanyakwa tena na Fofana.