Habari Mseto

Kenya yaimarisha miundomsingi ya kufanya biashara

November 1st, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Kenya imeimarika kwa nafasi 19 katika mazingira bora ya kufanya biashara ulimwenguni.

Ripoti hii ni kwa mujibu wa Benki ya Dunia. Kwa sasa, Kenya imo katika nafasi ya 61 katika uchunguzi huo, 2019.

Ripoti hiyo iliyotolewa Jumatano imeorodhesha Kenya kama ya saba miongoni mwa mataifa 10 yaliyoimarisha zaidi mazingira ya kufanya biashara.

Kenya iliimarika katika utoaji wa mikopo, ulinzi wa wawekezaji wadogo na uwezo wa kulipa ushuru kwa njia rahisi. Hii ni baada ya serikali kuunganisha vyeti vya kuidhinisha biashara ya mtu mmoja kuwa cheti kimoja.

Pia, serikali ilifanya njia ya kusuluhisha kufilisika kuwa rahisi kwa kuwawezesha wafanyibiashara kuendelea na biashara zao hata wanapotangazwa kufilisika huku kesi ikiendelea.

Hata hivyo, kupata vyeti vya kuidhinisha ujenzi ilikuwa vigumu, kusajili mali na kuanzisha biashara bado ni vigumu.