Habari MsetoMichezo

Kenya yaingia mduara wa medali voliboli ya ufukweni ya wanawake

June 22nd, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KENYA imeingia mduara wa medali kwenye voliboli ya ufukweni ya wanawake katika mashindano ya Bara Afrika ya ufukweni inayoendelea mjini Sal nchini Cape Verde.

Wachezaji Gaudencia Makokha na Naomie Too wamelipua wawakilishi wa Nigeria Nnoruga Tochukwu na Eyetsonetan Isabela kwa seti 2-0 za alama 21-13, 21-15 katika robo-fainali. Walikuwa wamelima Sierra Leone na Guinea-Bissau kwa seti 2-0 kila mmoja katika mechi za Kundi B.

Warembo wa Kenya, ambao walitumia dakika 45 kwa kubandua nje Wanigeria, wanaungana na wenyeji Cape Verde pamoja na Morocco na Namibia katika nusu-fainali.

Kenya haikuwa na bahati katika kitengo cha wanaume pale ilipolemewa na Msumbiji 2-1(21-18, 21-23, 15-7) katika robo-fainali.

Kenya haikuwa na bahati katika kitengo cha wanaume ilipolemewa na Msumbiji 2-1 (21-18, 21-23, 15-7) katika robo-fainali. Picha/ Hisani

Mechi za nusu-fainali za wanaume zitahusisha Angola, Msumbiji, Ghana na Morocco.

Ibrahim Odindo na James Mwaniki sasa watapigania nafasi za kuorodheshwa kutoka nafasi ya tano hadi nane.

Watakutana na Choaib Belhaj Salah na Mohamed Naceur kutoka Tunisia baadaye Jumamosi.

Fani ambazo Kenya inashiriki ni ‘kiteboarding’, Half Marathon, kupeleka mashua kwa kutumia mitumbwi, voliboli ya ufukweni, karate, soka ya ufukweni, handboli ya ufukweni, tenisi ya ufukweni na uogeleaji.

Charles Mneria Yosei alishindia Kenya medali ya fedha katika Half Marathon.

Mashindano haya yalianza Juni 14. Yatakamilika Juni 23.