Michezo

Kenya yaingia nusu fainali za Copa Africa, yasubiri TZ

December 4th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BAO la Mohammed Mbaruk kupitia penalti ya dakika ya 66, lilisaidia Kenya kuzamisha chombo cha Botswana kwenye mchuano wa robo fainali za Copa Africa hiyo Jumanne.

Mashindano hayo yanaendelea katika uwanja wa MPESA Foundation Academy, mjini Thika.

Ushindi huo wa 1-0 ulikatia Kenya tiketi ya nusu fainali dhidi ya Tanzania hii leo Jumatano.

Wavulana wa Kenya walijibwaga ugani ikiwa lazima washindi mechi hiyo, baada ya kupepetwa 3-1 na Zimbabwe katika mechi ya ufunguzi. Mechi ya pili Kenya waliwapokeza Msumbiji kichapo cha 3-0.

Utata uliotawala tukio lililochangia penalti ya Kenya ni suala lililomkera kocha wa Botswana, ambaye alikataa kuzungumza na wanahabari mwishoni mwa mechi.

Kwa upande mwingine, Tanzania walitoka nyuma bao moja na kuwaponda Uganda 6-2 katika robo fainali nyingine hapo jana.

Paul Nyerere aliwafungia Tanzania mabao matatu katika kivumbi hicho cha kusisimua.

Magoli mengine ya Tanzania, wanaonolewa na kocha Abel Mtweve, yalifumwa wavuni kupitia kwa Frank Sephania na Kassim Ibrahim aliyefunga mawili.

Chipukizi Abasi Kyeyune aliwafungia Uganda bao la pili baada ya ukurasa wao wa magoli kufunguliwa na Patrick Duke.

Wakicheza dhidi ya Zimbabwe, Kenya, ambao ndio mabingwa watetezi wa kombe hilo la Copa Africa, walifungiwa bao la kufutia machozi kupitia kwa nahodha Marcus Odhiambo.

Magoli ya Zimbabwe, waliowacharaza Namibia 4-1 katika robo fainali nyingine hapo Jumanne, yalijazwa kimiani na Luke Musiriki.

Kenya inawakilishwa na wavulana wa shule ya msingi ya Serani Boys chini ya kocha Daniel Lonje, katika makala ya Copa Africa mwaka 2019.

Dimba hilo halikuandaliwa mwaka 2018.

Katika robo fainali ya nne, kikosi cha Zambia kiliwapepeta Angola mabao 8-1 na hivyo kujikatia tiketi ya nusu fainali ya pili itakayowakutanisha leo na Zimbabwe.

Fainali ya kivumbi hicho cha wavulana chipukizi barani Afrika kitaandaliwa hapo Alhamisi.

Kinafadhiliwa na kampuni ya kutengeneza soda ya Coca-Cola.

Makala ya kwanza yalifanyika mjini Nakuru mwaka 2017.

Kenya waliwakilishwa na shule ya upili ya St Anthony’s Kitale Boys na Moi Girls Nangili. Vikosi vyote vilinyanyua ubingwa kwa upande wa wavulana na wasichana mtawalia.