Michezo

Kenya yaiondoa Zambia Copa Coca-cola U-16

December 14th, 2018 2 min read

NA RICHARD MAOSI 

DIMBA la Copa Coca-cola U-16 liliingia awamu ya nusu fainali Ijumaa katika uwanja wa Shule ya Wavulana Nakuru, mechi mbili zikiratibiwa kusakatwa.

Michuano uliosubiriwa kwa hamu ukiwa ni baina ya vijana wa St Antony Kitale wanaowakilisha Kenya na timu ya Zambia.

Kenya walingia uwanjani wakijivunia mashabiki wa nyumbani pamoja na kikosi dhabiti,ambacho hakijapoteza tangu michuano ianze rasmi.

Mshambulizi wa Botswana(kulia)akingangania mpira na Yusuf Faizal Seleman katika mchuano wa Copa Coca-cola Alhamisi katika uwanja wa shule ya wavulana ya Nakuru. Picha/Richard Maosi

Kufikia mechi ya Ijumaa Kenya ilikuwa na mfungaji bora Jacob Onyango aliyekua ametikisa nyavu mara 5,katika mechi mbili za awali

Mshambulizi Issa Rashid alishirikiana vyema na Christopher Raila dakika ya 22 walipopokezana mapasi safi ndani ya kisanduku lakini kipa wa timu ya Zambia David Miganja akaondosha mkiki na kuinusuru timu yake ilipoonekana kulemewa.

Kipindi cha kwanza kilimalizika sare tasa ya 0-0.Katika kipindi cha pili David Leon alifunga penalti,Aron Kibiwot alipoangushwa ndani ya kisanduku dakika ya 57,na kufanya mambo kuwa 1-0 kufikia mwisho wa kipindi cha pili.

Cedric Muchina (kushoto) wa Kenya aking’ang’ania mpira na mlinzi wa timu ya Uganda katika pambano la Copa coca cola 2018 katika shule ya wavulana ya Nakuru Alhamisi.Kenya ilishinda 1-0. Picha/Richard Maosi

Kwingineko Nigeria ilipata ushindi wa 5-1 dhidi ya Botswana.Mvua ya magoli ilianza dakika ya 15 kupitia kiungo Williams Gift.James Ogheretega aliongeza la pili dakika ya 38.Hussein Mohammed na Henry Williams waliongeza la tatu nne na tano dakika ya 44,59,62 mtawalia.

Kenya itakutana na Nigeria uwanjani Afraha Siku ya Jumamosi.Mkufunzi Peter Mayoyo alisema anatarajia kunyanyua kombe la Copa awamu hii akionekana kuridhika na vijana wake wanaotesa

Kabla ya hapo siku ya Alhamisi kulikuwa na michuano hiyo ya Copa Coca-cola awamu ya robo fainali ambapo Botswana walishinda Msumbiji 4-3 kupitia mikwaju ya penalti muda wa kawaida ulipomalizikia 1-1.

Rickson Ngambi (kulia) wa Zambia akishindana ubabe na Aron Kibiwot wa Kenya katika michuano ya Copa coca cola uwanja wa shule ya upili ya Nakuru Picha/Richard Maosi

Mechi ilianza kwa kasi Msumbiji wakipata bao la mapema kunako dakika ya kwanza kupitia juhudi za mchezaji Hussein Alberto .

Botswana walisawazisha dakika ya 51 kupitia mkwaju wa ikabu uliochongwa na Eric Pono nje ya kisanduku na kuwahakikishia Black Zebras nafasi ndani ya nusu fainali.

Aidha Nigeria walilazimika kusubiri hadi kipindi cha pili kuvuna ushindi wa 2-1 dhidi ya Afrika kusini.Hillongwane Njabulo alitangulia kufungia Afrika kusini dakika ya kwanza lakini Nigeria wakasawazisha na kupata bao la ushindi kupitia Gift Williams na Daniel Chibuke dakika za 35 na 58 mtawalia.

Kikosi cha Kenya wakipasha misuli moto kabla ya kupambana na Botswana katika michuano ya Copa coca cola siku ya Jumatano katika uwanja wa shule ya wavulana ya Nakuru.Kenya ilifuzu hatua ya mwondoano. Picha /Richard Maosi