Kimataifa

Kenya yaionya Tanzania kwenye mzozo wa pipi

May 17th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Kenya imeipa makataa ya wiki mbili serikali ya Tanzania kufanyia udadisi bidhaa za Kenya kubainisha ikiwa zinatengenezwa kwa sukari iliyoagizwa kutoka nje.

Hii ni baada ya mgogoro kuibuka ambapo Tanzania ilizuia peremende za Kenya zisizotozwa ushuru kuingia nchini humo.

Sasa serikali ya Kenya imeonya kuwa itazuia kuingia kwa bidhaa kutoka Tanzania nchini ikiwa Tanzania haitabadilisha mwenendo wake.

Hii ni baada ya serikali ya John Pombe Magufuli kutoza ushuru wa asilimia 25 kwa peremende zisizotozwa ushuru kutoka Kenya nchini humo katika mgogoro uliozuka Machi.

Baadhi ya vitu vingine vilivyozuiwa kuingia Tanzania ni sharubati, isikrimu na pipi za kutafuna.

Tanzania ilisema kuwa bidhaa hizo za Kenya zilikuwa zikitengenezwa kwa kutumia sukari ya kuagiza kutoka nje ya nchi, ambayo haina ushuru.