Kenya yakopa Sh80b baada kutangaza bajeti ya madeni

Kenya yakopa Sh80b baada kutangaza bajeti ya madeni

Na PAUL WAFULA

BENKI ya Dunia jana iliipatia Kenya mkopo mwingine wa Sh80.2 bilioni kwa lengo la kukabiliana na janga la Covid-19 na kufufua mageuzi katika taasisi za kitaifa zikiongozwa na kampuni ya kusambaza umeme Kenya Power.

Mkopo huo ulitolewa siku moja tu baada ya Waziri wa Fedha Ukur Yatani kusoma bajeti mpya ya Sh3.6 trilioni ambayo serikali haitaweza kuimudu ikiwa Bunge halitaidhinisha ombi lake la kuongeza kiwango chake cha madeni ambacho kwa sasa ni Sh9 trilioni.

Taasisi hiyo ya Bretton Woods ilisema jana kuwa, mkopo huo utasaidia kuimarisha mikakati thabiti ya kiuchumi nchini inayotumia kawi salama kwa mazingira, kupata nafuu kutokana na janga la Covid-19.

Ilisema kuwa fedha hizo zitafadhili mageuzi ya kisera ambayo yataimarisha uwazi na uwajibikaji katika michakato ya idara za kutoa kandarasi za serikali na kuimarisha matumizi mwafaka ya uwezekezaji wa fedha za umma.

“Sera hii ya maendeleo inaunga mkono mikakati ya kuimarisha ustawishaji wa madeni ya wastan kupitia uwazi zaidi na uwajibikaji katika matumizi ya serikali, kuimarisha ufadhili unaoendelea wa Benki ya Dunia ili kuimarisha mifumo ya kusimamia fedha za umma,” lilisema shirika hilo la kimataifa kupitia taarifa.

Shirika hilo lilisema kuwa, mkopo huo utasaidia kubuniwa kwa tasnia ya kutoa kandarasi kielektroniki kwa sekta ya umma kwa lengo la kufanya mchakato wa serikali wa kutoa kandarasi kuhusu bidhaa za umma kuwa na uwazi. “Hii itasaidia kuongeza uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma na kupunguza ufisadi.

Ufadhili huu pia utaimarisha usimamizi kuhusu uwekezaji wa fedha za umma kwa kupunguza gharama na kutumia utaratibu wa kina katika uteuzi, kuangazia na kutathmini miradi yote,” ilisema.Shirika hilo lilisema kwamba, mikakati hiyo inatarajiwa kutoa mazao ya akiba kiasi cha hadi Sh278 bilioni.

  • Tags

You can share this post!

Kalonzo, Raila kufufua NASA

Njama ya serikali kuandaa refarenda yafichuka