Michezo

Kenya yamaliza nafasi ya 14 michuano ya ufukweni Afrika

June 24th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KENYA ilikamilisha makala ya kwanza ya mashindano ya Bara Afrika ya ufukweni katika nafasi ya 14 kati ya mataifa 54 yaliyokusanyika mjini Sal nchini Cape Verde kutoka Juni 14-23, 2019.

Timu ya Kenya ilizoa nishani moja ya fedha kupitia kwa mkimbiaji Charles Yosei Mneria (mbio za kilomita 21) na shaba mbili zilizopatikana kupitia kwa Fazal Khana na Ibrahim Kibet (tenisi ya wachezaji wawili kila upande) na wanavoliboli Gaudencia Makokha na Naomie Too.

Medali ya mwisho ya Kenya ilipatikana katika siku ya mwisho pale timu ya Kenya (Makokha na Too) ilinyamazisha wenyeji Janice Varela na Ludmila Varela kwa seti 2-0 za alama 21-6, 21-11 katika mechi ya kutafuta nambari tatu iliyodumu saa moja.

Wakenya walikamilisha kitengo hiki na ushindi tano kati ya mechi sita ilizocheza. Ilichapa Sierra Leone, Guinea-Bissau na Nigeria kwa seti 2-0 kila mmoja kabla ya kupokea dozi sawa na hiyo kutoka kwa Namibia katika nusu-fainali Juni 22. Ilijikakamua na kuzidia wanavisiwa wa Cape Verde katika mechi ya kutafuta medali ya shaba.

Ilimaliza soka katika nafasi ya sita baada ya kulimwa 10-6 na Algeria.

Katika mbio za kilomita 21, Mneria alimaliza wa pili nyuma ya Robert Chemonges (Uganda) na mbele ya raia wa Djibouti Bouh Moumin kwenye kitengo cha wanaume naye Florence Malyunga akiridhika katika nafasi ya nne nyuma ya Senani Reham (Algeria), Lavinia Haitope (Namibia) na Priscilla Chelangat (Uganda) kwa upande wa wanawake.

Katika makala haya ya kwanza, Kenya pia ilizoa medali ya shaba katika tenisi ya wachezaji wawili kila upande kupitia kwa Fazal Khan na Ibrahim Yego.

Kenya iliambulia pakavu katika fani za ‘kiteboarding’, kupeleka mashua kwa kutumia mitumbwi, karate, soka, handboli na uogeleaji. Mashindano haya yalivutia washiriki 1,000 kutoka mataifa 54.

MSIMAMO WA BARA AFRIKA

Taifa Dhahabu Fedha Shaba Jumla

Morocco 9 3 4 16

Algeria 5 6 5 16

Tunisia 3 3 1 7

Cape Verde 3 2 5 10

Mauritius 2 2 0 4

Mali 2 1 1 4

Nigeria 1 2 4 7

Uganda 1 0 1 2

Msumbiji 1 0 0 1

Senegal 1 0 0 1

Namibia 0 4 0 4

Togo 0 2 0 2

Botswana 0 1 3 4

Kenya 0 1 2 3

Ghana 0 1 0 1

Ivory Coast 0 0 3 3

Burundi 0 0 1 1

Djibouti 0 0 1 1