Michezo

Kenya yanyeshea Zanzibar 5-0 U-20

September 22nd, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

RISING Stars ya Kenya imechukua uongozi wa Kundi B kwenye mashindano ya soka ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 baada ya kubebesha Zanzibar mabao 5-0 uwanjani Njeru nchini Uganda, Jumapili.

Mshambuliaji wa Kariobangi Sharks, Sydney Lokale alikuwa shujaa wa Kenya alipopachika mabao manne katika mchuano huu wa Kundi B. Alifungua ukurasa wa mabao baada ya Kenya kupata penalti dakika ya 32 na kuongeza la pili dakika sita baadaye.

Lokale hakukosea tena kutoka kwa kitovu cha penalti baada ya kubeba majukumu hayo nahodha wa Zanzibar, Mustapha Muhsin Juma alipolishwa kadi nyekundu. Alipata bao la nne dakika ya 80 kabla ya Austin Otieno Odhiambo kufunga ukurasa wa mabao dakika ya 83.

Vijana wa kocha Stanley Okumbi sasa wako juu ya jedwali kwa alama tatu, sawa na Tanzania, ambayo pia ilianza kampeni yake kwa kishindo ilipolipua Ethiopia 4-0 mapema katika uwanja huu. Andrew Albert Simchimba alifungia Tanzania mabao matatu naye John Kelvin Pius akacona lango mara moja.

Katika siku ya kwanza ya mashindano haya mnamo Septemba 21, wenyeji Uganda Hippos walikabwa na Eritrea 1-1 uwanjani Pece. Ivan Bogere alifungia Hippos katika dakika ya 37 naye Yosief Tesfai Mewael akasawazishia Eritrea dakika 20 baadaye katika mechi hii ya Kundi A.

Nayo Burundi ilitoka 3-3 dhidi ya Sudan Kusini katika mechi ya Kundi C. Burundi ilitikisa nyavu kupitia kwa Yassin Dushime, Karim Niyonkuru na Hakim Hakizimana naye Daniel Lual Gumnok akafungia Sudan Kusini mabao yote matatu.

Ratiba ya Septemba 23: Burundi na Sudan Kusini (2pm), Eritrea na Sudan (2pm), Djibouti na Uganda (4pm).