Michezo

Kenya yaona vimulimuli tenisi ya Afrika Mashariki

March 4th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KENYA ilianza kampeni yake katika mashindano ya tenisi ya Afrika Mashariki vibaya baada ya kupoteza kwa mechi 3-0 dhidi ya Burundi jijini Kigali, Rwanda, Jumapili.

Katika kitengo cha mchezaji mmoja mmoja cha wavulana wasiozidi umri wa miaka 12, Liberty Baraka Kibue alipepetwa 6-2, 6-1 na Abdoul Shakur Malick naye Raqeem Virani akazabwa 6-0, 6-3 na Abdilah Ndayishimiye.

Ushirikiano wa Malick na Ndayishimiye pia uliwazidi Kibue na Virani nguvu 6-1, 6-3.

Wawakilishi wa Kenya katika kitengo cha wasichana wasiozidi umri wa miaka 12, Anouk Vandevelde, Reha Kipsang’ na Debbie Polo wataingia uwanjani Jumatatu kukabiliana na wenyeji Rwanda. Timu ya Kenya inanolewa na Caroline Oduor.

Mataifa manne yanashiriki mashindano haya. Mbali na Kenya, Rwanda na Burundi, Uganda pia inashiriki. Tanzania ilijiondoa dakika ya mwisho kutokana na ukosefu wa udhamini.

Mashindano haya yalianza Machi 4 na yatakamilika Machi 8, 2018.