Kenya yapitisha marekebisho ya Sheria ya Pufya

Kenya yapitisha marekebisho ya Sheria ya Pufya

Na CHARLES WASONGA

MASENETA Jumanne walipitisha kwa kauli moja Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Kupambana na Matumizi ya Dawa za Kusisimua Misuli miongoni mwa wanaspoti almaarufu pufya.

Uovu huo umekithiri zaidi miongoni mwa wanariadha nchini hali ambayo imechangia baadhi yao wenye haiba kubwa kimataifa kupigwa marufuku kushiriki mashindano ya humu nchini na kimataifa.

Mswada huo umesheheni vipengele vinavyooanisha sheria za kupambana na matumizi ya dawa hizo nchini (Anti-Doping Act, 2016 na kanuni za Shirika la Kimataifa la Kupambanana na Matumizi ya Dawa za Kusisimua Misuli (World Anti-Doping Agency-WADA.

Kenya ilitarajiwa kutimiza lengo hilo kufikia Desemba 31, 2020 wakati ambapo Mswada huo unapasa uwe umetiwa saini na Rais Uhuru Kenyatta.

Mswada huo ulipitishwa na Bunge la Kitaifa mnamo Desemba 22, 2020. Kenya ni taifa linalotambuliwa na kusifiwa kwa kuwa na wanariadha wenye talanta za kipekee haswa katika mbio za masafa marefu. Ushindi wao katika mashindano ya kimataifa umeiletea Kenya sifa na heshima katika mida ya kimataifa.

Hata hivyo, ongezeko la visa vya matumizi ya dawa za kuongeza nguvu zilizoharamishwa miongoni mwa wanariadha wa Kenya katika miaka michache iliyopita imeiletea Kenya sifa mbaya katika fani hiyo ya spoti.

Tayari zaidi ya wanariadha 50 wa Kenya, miongoni mwao wakiwa ni wale waliong’aa katika mashandano ya Olimpiki kama vile Asbel Kiprop na Jemimah Sumgong, wamepigwa marufuku kushiriki mashindani ya riadha humu nchini na ulimwenguni kwa vipindi tofauti kwa kupatikana wametumia dawa hizo.

Kiprop alishinda mbio ya mita 1,500 katika mashindano ya Olimpiki ya 2008 huku Sumgong akishinda katika mbio za marathon katika Olimpiki ya 2016.

Wengine waliopigwa marufuku kwa kupatikana wametumia dawa ni Mshindi wa Dunia katika mbio za mita 1,500 mnamo 2017 Elijah Managoi, aliyekuwa Bingwa wa Dunia katika Mbio za Marathon Wilson Kipsang, Daniel Wanjiru (aliyekuwa Bingwa wa London Marathon) na Rita Jeptoo ambaye ni Bingwa wa zamani wa Boston na Chicago Marathon kwa Wanawake.

Rais Kenyatta sasa anatarajiwa kutia saini mswada huu kabla ya Desemba 31,2020 ili Kenya isifungiwe nje ya mashindano ya kimataifa.

Hii ni kwa sababu Kenya ilitia saini mkataba wa Unesco unaopinga matumizi ya dawa katika spoti mnamo 2009. Kwa hivyo, ilikuwa mojawapo ya mataifa wanachama wa mkataba huo na unashurutishwa kutekeleza kanuni ya kimataifa kuhusu vita dhidi ya matumizi ya dawa hizo zilizoharamishwa.

Kanuni mpya kuhusu vita dhidi ya uovu huu itaanza kutekelezwa mnamo Januari 1, 2021 ambayo imeanzisha viwango vipya katika mapambano dhidi ya matumizi ya dawa hizo.

You can share this post!

Wabunge wataka CDF iongezwe kujenga madarasa

Usiwatambue Wapemba kwa vilemba pekee, wana sifa nyingine...