Michezo

Kenya yapoteza mechi ya pili magongo ya kutafuta tiketi Olimpiki 2020

August 13th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MATUMAINI ya wanaume wa Kenya kurejea katika Olimpiki katika fani ya mpira wa magongo mwaka 2020 yamedidimizwa zaidi baada ya kupoteza mechi ya pili kwenye mchujo wa Afrika kwa kucharzwa 7-2 na Misri katika Chuo Kiku cha Stellenbosch nchini Afrika Kusini, Jumanne.

Kenya ilifungwa mabao matatu ya haraka kabla ya kugutuka ilikuwa chini mabao 4-0 wakati wa mapumziko baada ya kufungwa na Mohamed Adel dakika ya tatu na saba, Ahmed El-Ganaini dakika ya sita na Amr Ibrahim dakika ya 24.

Kenya ilijikakamua katika kipindi cha pili na kupunguza mwanya huo kupitia kwa Constant Wakhura dakika ya 33 baada ya kupata kona fupi. Kabla hata ya kusheherekea bao hilo, Misri iliongeza bao la sita Hossam Ghobram na lingine kutoka kwa Ahmed Gamal dakika ya 37.

Festus Onyango alifungia Kenya bao la pili dakika ya 40 kabla ya Misri kufunga ukurasa wa magoli kupitia kwa El-Ganaini.

Kichapo hiki ni cha pili mfululizo kwa Kenya iliyotupa uongozi mara mbili ikipepetwa 3-2 na Ghana katika mechi yake ya ufunguzi mnamo Agosti 12. Inamaanisha kuwa Kenya sasa itakuwa ikitafuta tu kujiondolea fedheha itakapokutana na Zimbabwe (Agosti 15), Afrika Kusini (Agosti 17) na Namibia (Agosti 18) katika mechi zake tatu zilizosalia.

Misri, ambayo ilikutana na Kenya siku moja baada ya kupepeta Zimbabwe 6-0, imejiweka pazuri kufuzu.