Michezo

Kenya yapoteza mwanariadha mwingine, Charles Kipsang

February 25th, 2024 1 min read

NA LABAAN SHABAAN

KENYA imefiwa na mwanariadha mwingine, Charles Kipsang Kipkorir, majuma mawili baada ya kifo cha mshikilizi wa rekodi ya marathon duniani Kelvin Kiptum.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Xinhua, Kipsang alifariki Jumamosi, Februari 24, 2024 nchini Cameroon.

Alianguka na kufa muda mfupi baada ya kumaliza mashindano ya riadha.

Kulingana na vituo vya habari Cameroon, Kipsang alikuwa anashiriki makala ya 29 ya Mount Cameroon Race of Hope.

Alikata roho wakati akiendelea kupokea huduma za dharura hospitalani.

Wakati wa mashindano, Kipsang alikuwa anaongoza kabla ya kukumbwa na matatizo akikaribia utepe.

Alimaliza mbio akiwa nafasi ya 16 kama ilivyothibitishwa na Gavana wa Cameroon Bernard Okalai Bilia.

Madaktari waliokuwa ugani Molkyo walimfanyia huduma za dharura kumpa nguvu Kipsang kabla ya kumhamisha hadi Hospitali ya Buea Regional.

Akizungumzia tukio hili, Gavana Bilia alishindwa kueleza bayana chanzo cha kifo hicho.

“Hatuwezi kusema hasaa nini kilifanyika. Tunaweza kuamini pengine ni mshtuko wa moyo.”

Kisha akaongeza: “Walimpeleka hospitali ya kanda. Alikuwa tayari amefariki”.

Ushiriki wa Kipkorir katika mbio za Mount Cameroon Race of Hope uliashiria tukio muhimu.

Kipkorir amekuwa mwanariadha wa kwanza kujisajili katika shindano la kimataifa kongwe zaidi Afrika.

Katika umri wa miaka 33, mwendazake alionekana kuwa katika kilele.

Aliwahi kudhihirisha kipaji chake katika mbio kadhaa duniani zikiwemo mashindano ya masafa marefu ya Bali, the Kuala Lumpur na Casablanca.

Kifo hiki kimejiri majuma mawili baada ya Kenya kumpoteza mwanariadha mwingine wa hadhi ya juu Kelvin Kiptum.

Kiptum alifariki katika ajali akiwa na kocha wake Gervais Hakizimana.

Alizikwa kaunti ya Elgeyo Marakwet Ijumaa, Februari 23, 2024 katika mazishi yaliyowaleta pamoja viongozi wa hadhi ya juu serikalini na duniani, akiwemo Rais William Ruto, naibu wake, Rigathi Gachagua na Mkuu wa Mwaziri, Musalia Mudavadi.