Michezo

Kenya yapoteza tena Dubai Sevens

December 6th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MATUMAINI ya timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Kenya ya wanaume almaarufu Shujaa kufika robo-fainali kuu kwenye Raga za Dunia, duru ya Dubai Sevens, yamezimwa baada ya kupigwa 12-5 na Uingereza, Ijumaa.

Kichapo hiki kilikuwa cha pili mfululizo kwa Kenya kwenye Kundi D baada ya kulemewa na Afrika Kusini 19-12 siku ya Alhamisi.

Kenya, ambayo ilihitaji ushindi dhidi ya Uingereza kuweka hai matumaini yake, ilizamishwa na Waingereza kupitia kwa miguso ya Oliver Lindsay-Hague na Daniel Bibby na mkwaju kutoka kwa Tom Emery. Nelson Oyoo alifungia Kenya ya kocha Paul Feeney mguso wa kufutia machozi.

Shujaa itakamilisha mechi zake za makundi dhidi ya Uhispania saa kumi na mbili na nusu baadaye leo

Katika mechi zingine zilizosakatwa leo Ijumaa, Samoa ilitinga robo-fainali kutoka Kundi C baada ya kuzaba Wales 31-12. Wanavisiwa wa Samoa walikuwa wamelima Canada 19-12 katika siku ya kwanza.

New Zealand pia ilijikatia tiketi ya robo-fainali kutoka kundi hili baada ya kulipua Canada 31-7 na Wales 36-7.

Australia iko ndani ya mduara wa nane-bora baada ya kupepeta Scotland 43-14 na Ireland 45-21 katika Kundi B, ambalo pia vijana wa Marekani ya Mike Friday walisonga mbele kufuatia ushindi wao dhidi ya Ireland 24-19 na Scotland 31-21.

Kundi A lingali wazi licha ya kuwa Ufaransa imechabanga Japan 41-5 na Argentina 12-10. Fiji ilihatarisha kampeni yake baada ya kuzamishwa 24-21 na Argentina katika mechi yake ya pili. Wafiji, ambao walilipua Japan 24-17 katika mechi yao ya ufunguzi, lazima wapige Ufaransa na kuomba Argentina ichapwe na Japan, ingawa kuna uwezekano mkubwa tofauti ya ubora wa magoli ndio itaamua timu mbili zitakazosonga mbele kutoka kundi hili. Uingereza pia imeingia robo-fainali baada ya kuchapa Kenya na Uhispania.