Kenya yasajili visa vipya 1,259 vya Covid-19 kufikisha idadi jumla ya 203,213

Kenya yasajili visa vipya 1,259 vya Covid-19 kufikisha idadi jumla ya 203,213

Na CHARLES WASONGA

KWA mara ya kwanza ndani ya miezi miwili iliyopita Kenya, Jumamosi imenakili visa 1,259 vipya vya maambukizi ya corona, idadi ya juu zaidi kuwahi kurekodiwa ndani ya kipindi cha miezi mwili ambayo imepita.

Visa hivyo vimegunduliwa baada ya sampuli 8,081 kufanyiwa uchunguzi ndani ya muda wa saa 24 zilizopita, na hivyo kuashiria kiwango cha maambukizi cha asilimia 15.6.

Kulingana na taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Jumamosi, idadi jumla ya visa vya maambukizi sasa ni 203,213 baada ya jumla ya sampuli 2,132,355 kufanyiwa vipimo.

Visa vipya vya maambukizi vimesambaa katika kaunti mbalimbali jinsi ifuatavyo; kaunti ya Nairobi inaongoza kwa visa 417, Nyeri (139), Kiambu (120), Mombasa (96), Nakuru (66), Kilifi (60) , Kajiado (42) , Uasin Gishu (34), Taita Taveta (31), Nandi (28), Busia (21), Machakos (19), Kericho (16), Embu (16), na Nyandarua imeandikisha visa 15.

Kaunti za Kirinyaga na Kwale nazo zimeandikisha visa 13 kila moja, Trans Nzoia (11), Kisumu (10), Murang’a (10), Turkana (9), Baringo (8), Tana River (7), Bomet (7), Meru (6), Garissa (5) nazo kaunti za Siaya, Bungoma, Homa Bay, Migori, Narok, Nyamira, na Kakamega zikiripoti visa vinne kila moja.

Kwa upande mwingine, Kaunti ya Vihiga imeripoti visa vitatu huku Kisii, Kitui na Makueni zikiandikisha visa viwili kila moja huku Pokot Magharibi na kaunti jirani ya Elgeyo Marakwet zikirekodi kisa kimoja kila moja.

Wakati huo huo, idadi ya wagonjwa waliofariki kutokana na Covid-19 kufikia Jumamosi imefika 3,931 baada ya wengine watano kufa ndani ya saa 24 zilizopita.

Idadi ya wagonjwa waliopona ni 498,357 wakiwa ni wale waliokuwa wakihudumiwa nyumbani huku 141 wakiwa ni wale ambao walikuwa wamelazwa katika hospitali mbalimbali nchini.

Idadi hiyo inafikisha 188,936 idadi jumla ya wagonjwa waliopona corona tangu mwaka 2020.

Wizara ya Afya pia ilisema kuwa kufikia Jumamosi, jumla ya wagonjwa 1,469 wamelazwa katika hospitali mbalimbali nchini huku 3,965 wakitunzwa nyumbani.

Vile vile, jumla ya wagonjwa 185 wamelazwa katika vyumba vya kuwahudumia wagonjwa mahututi 83 wakisaidiwa kupumua na 86 wakiongezewa hewa ya oksijeni.

You can share this post!

Jamaica yazoa medali zote tatu za Olimpiki katika mbio za...

Pochettino matumaini juu PSG ikigaragazana na Lille katika...