Makala

Kenya yashauriwa kujiondoa katika mpango wa kurejesha amani Haiti

March 12th, 2024 3 min read

NA CHARLES WASONGA

MASWALI yameanza kuibuliwa kuhusu hatima ya mpango wa Kenya kuwapeleka polisi 1,000 nchini Haiti kurejesha amani kufuatia kujiuzulu kwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo Ariel Henry.

Hii ni baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki kushikilia kuwa Kenya itawapeleka maafisa hao Haiti “hivi karibuni”.

“Sasa tuko katika awamu ya maandalizi. Mipango mingine yote iko tayari ikiwemo mkataba wa usalama, sheria za kukamatwa na kuzuiliwa kwa wahalifu na namna ya kutekeleza sheria hiyo,” Prof Kindiki akasema Jumatatu akiwa mjini Machakos.

Waziri huyo alifafanua kuwa ni maafisa wa polisi kiume pekee watakaopelekwa kupambana na magenge ya walifu katika taifa hilo la eneo la Caribbean.

Lakini sasa mchanganuzi wa masuala ya usalama George Musamali anasema kuwa kujiuzulu kwa Henry kutafanya hali ya usalama nchini Haiti kuwa tete zaidi na hivyo hatari kwa ujio wa maafisa wa kigeni  wa kulinda amani.

“Hali ya usalama nchini Haiti itakuwa hata mbaya zaidi kufuatia shinikizo za kuwataka wakuu wa polisi kujiuzulu. Kwa hivyo, hamna haja kwa Kenya kutuma maafisa wake wa polisi katika mazingira ya machofuko na ukosefu wa uongozi kama yalivyo katika taifa hilo,” akaeleza.

Mtaalamu huyo sasa anashauri jamii ya kimataifa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) kuandaa mchakato mpya wa kurejesha utulivu nchini Haiti.

“Hii ni kwa misingi ya kudorora kwa usalama kiasi kwamba Amerika inayounga mkono mpango huo, imeshauri raia wake wote kuondoka Haiti,” akaeleza Bw Musamali.

Mtaalamu wa masuala ya usalama George Musamali. PICHA | MAKTABA

Kwa upande wake, kiongozi wa chama cha Thirdways Alliance Ekuru Aukot sasa anamtaka Rais William Ruto kuweka kando kabisa mpango wa kuwapeleka polisi wa Kenya nchini Haiti.

“Ni kinaya kwamba Amerika, kupitia Waziri wa Masuala ya Kigeni Anthony Blinken, inaishinikiza Kenya kupeleka polisi Haiti huku ikiondoa raia na maafisa wa ubalozi wake katika taifa hilo. Kufuatia kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Ariel Henry na kukithiri kwa vita nchini humo, Kenya inafaa kujiondoa kabisa katika mpango wa kuleta amani nchini humo hadi jamii ya kimataifa itakapoingilia kati na kutuliza hali,” Bw Aukot akaambia Taifa Leo mnamo Jumanne kwenye mahojiano kwa njia ya simu.

Henry aliwasilisha barua ya kujiuzulu mnamo Jumatatu baada ya mkutano wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya eneo la Caribbean (CARICOM).

Hii ni kulingana na taarifa kutoka kwa mwenyekiti wa CARICOM Mohammed Irfaaan Ali, ambaye ni rais wa taifa la Guyana.

“Tunatambua kujiuzulu huku kunafaa kufuatiwa na kuundwa kwa baraza la mpito la urais na kutajwa kwa Waziri Mkuu wa muda,” Irfaan akaeleza.

Viongozi wa jumuiya ya CARICOM walikutana na viongozi kutoka nchi nyingine zikiwemo Amerika na Canada mnamo Jumatatu huku hali ya usalama ikiendelea kudorora zaidi nchini Haiti.

Duru zilisema kuwa mkutano huo uliamua kwamba jopo la urais la wanachama saba liteuliwe na ambalo litateua kaimu waziri mkuu kuongoza katika kipindi cha mpito.

Aidha, waziri huyo mkuu wa muda kwa usaidizi wa waangalizi wawili atasimamia uchaguzi wa urais ili kujeresha utawala wa kidemokrasia nchini Haiti.

“Sote tunakubaliana kwamba Haiti inaelekea kutumbukia katika janga kubwa. Sharti tuchukue hatua ya haraka ili kurejesha utulivu na kurejesha nchi hiyo kwa raia wa Haiti,”  Irfaan akawaambia wanahabari.

“Maamuzi magumu tunayofanya leo ni yanaendeleza masilahi ya watu wa Haiti,” akaongeza.

Aidha, duru zilisema kuwa waziri mkuu huyo wa muda, ambaye hajateuliwa, pia atatarajiwa kuweka maandalizi ya kuwasilisha kwa vikosi vya usalama kutoka mataifa ya kigeni (MNSSM) vikiongozwa na maafisa wa polisi wa Kenya.

Henry alijiuzulu baada ya ziara yake ya hivi majuzi nchini Kenya ambapo alishindwa kurejea Haiti.

Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry akiwa katika Chuo Kikuu cha USIU-Africa jijini Nairobi mnamo Machi 1, 2024. PICHA | SILA KIPLAGAT

Baadaye alilazimika kutafuta hifadhi jijini Puerto Rico katika taifa jirani la Jamhuri ya Dominican.

Hii ni baada ya mapigano kuchacha nchini Haiti baada ya magenge ya wahalifu kushambulia uwanja wa ndege wa kimataifa ili kuzuia kutua kwa ndege iliyombeba Henry.

Aidha, walivamia gereza lenye ulinzi mkali Haiti na kuwaachilia huru zaidi ya wafungwa 4,000.

Wanachama wa magenge hayo, wakiongozwa na kiongozi wa genge la Revolution G9 Jimmy Cherizier almaarufu ‘Barbecue’, wamekuwa wakishinikiza kujiuzulu kwa Henry wakimlaumu kwa kudinda kuitisha uchaguzi wa urais.

Polisi wa zamani Jimmy ‘Barbecue’ Cherizier, kiongozi wa genge la ‘G9’, ashika simu yake baada ya kuwahutubia wanahabari katika eneo la Delmas 6, Port-au-Prince, Haiti mnamo Machi 5, 2024. PICHA | REUTERS