Habari Mseto

Kenya yasifiwa kupunguza vifo vya watoto wachanga

September 22nd, 2019 2 min read

Na PAUL REDFERN

KENYA imepiga hatua katika juhudi zake za kupunguza vifo vya watoto wachanga walio chini ya umri wa miaka mitano katika miaka 25 iliyopita. Haya ni kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa na Benki ya Dunia (WB).

Ripoti hiyo inasema kuwa vifo hivyo vimepungua hadi kufikia watoto 41 kati ya 1,000 ilhali kiwango cha vifo hivyo duniani ni 39 kati ya watoto 1,000.

Mnamo 1996 idadi ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano waliofariki ilikuwa 114 kati ya watoto 1,000, hali inayoashiria kuwa vifo hivyo vimepungua kwa kiwango cha asilimia 60 kwa kipindi cha miaka mitatu.

Na idadi hiyo ni chini zaidi ikilinganishwa na idadi wastani ya vifo vya watoto wachanga katika mataifa yote yaliyoko kusini mwa jangwa la Sahara.

Ingawa Kenya ingali na nafasi ya kupiga hatua zaidi, takwimu za hivi punde ni bora zaidi ikilinganishwa na zile za mataifa kadhaa ya Afrika.

Mataifa ya Somalia, Nigeria, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sierra Leone na Guinea ni miongoni mwa mataifa yenye viwango vya juu vya vifo vya watoto wachanga barani Afrika ambapo ni zaidi ya watoto 100 kati ya 1,000.

Benki ya Dunia inasema kwamba licha ya Kenya kuandikisha rekodi nzuri, hali si nzuri katika mataifa yaliyoko Kusini mwa jangwa la Sahara.

Mnamo mwaka wa 2018 mtoto mmoja kati ya 10 wenye umri wa miaka mitano kuenda chini walifariki katika Afrika ikilinganishwa na mtoto mmoja kati ya 24 katika mataifa yaliyoko kusini mwa bara Asia. Hii ina maana kuwa Afrika na Asia ndio waliongoza kwa vifo vya watoto wachanga mwaka huo.

Umri

Ripoti hiyo pia inasema kuwa asilimia 40 ya vifo vya watoto walioko chini ya umri wa miaka 15 hutokea kuanzia mwezi wa kwanza baada ya wao kuzaliwa.

Inakisiwa kuwa jumla ya watoto 2.5 milioni kote duniani walifariki mwezi mmoja baada ya kuzaliwa mnamo mwaka wa 2018. Kiwango hicho ni sawa na watoto 7,000 wachanga kila siku.

Aidha, imebainika kuwa idadi ya watoto ambao hufariki wakiwa na umri mdogo inapungua kwa kasi kuliko idadi ya watoto wanaofariki wakiwa na umri mkubwa.