Kenya yasifiwa kutumia teknolojia kuzuia kuenea kwa corona JKIA

Kenya yasifiwa kutumia teknolojia kuzuia kuenea kwa corona JKIA

NA LEONARD ONYANGO

UMOJA wa Afrika (AU) kupitia asasi yake ya kiafya ya Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) umeipongeza Kenya kwa kuwa miongoni mwa mataifa ya kwanza barani kuanza kutumia teknolojia yake ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Uvumbuzi huo ambao unarahisisha mchakato wa kuthibitisha matokeo ya vipimo vya corona na uhalisia wa chanjo za virusi hivyo, tayari umeanza kutumiwa na Wizara ya Afya humu nchini.

“Wizara yetu imeshirikiana na AU na Africa CDC, kwa usaidizi wa kiteknolojia kutoka PanaBIOS kutekeleza mfumo wa mitandaoni wa kuthibitisha vyeti vya vipimo vya corona kwenye maabara,” Bw Mutahi Kagwe, Waziri wa Afya amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa Africa CDC Dkt John Nkengasong ameimiminia sifa Kenya kwa hatua hiyo ambayo Umoja wa Afrika unaamini utahakikisha usalama wa kiafya katika viwanja vya ndege, na hivyo kuwapa abiria imani ya kusafiri katika mataifa mbalimbali ya Afrika.

“Kenya imekuwa mstari wa mbele katika masuala ya kiteknolojia hapa barani, lakini ni juhudi zake katika mchakato mzima wa kuunganisha Afrika ambazo zinafanya ushirikiano wetu katika teknolojia za suluhu za kiafya kuwa ubunifu wa kutegemewa,” aliambia Taifa Leo.

Hapo Oktoba mwaka uliopita, AU ilizindua jukwaa la mtandaoni kwa jina Trusted Travel kama mojawapo ya suluhu za kuhakikisha biashara imeendelea Afrika, katika kongamano la mawaziri wa afya, uchukuzi na mawasiliano wa mataifa ya Afrika.

Suluhu hiyo iliyotengenezwa na shirika la PanaBIOS na kampuni tajika ya Zimbabwe Econet kwa sasa inatumika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kuwapima na kuwapa vyeti vya usafiri abiria wanaoingia humu nchini na wale wanaoondoka.

Antonia Filmer, raia wa Uingereza aliyesafiri Kenya majuzi ameelezea jinsi suluhu hiyo inawachangamsha Wakenya wakati ambapo raia katika mataifa ya bara Ulaya wanaonekana kugubikwa na huzuni.

“Nilipotua JKIA kabla ya kuingia kwa ofisi za uhamiaji, tulipigwa skeni na kupewa vyeti vya corona vya kuruhusiwa kuwa Kenya huku pia tukipimwa joto mwilini iliyounganishwa na kamera. Mchakato mzima ulichukua dakika 15 pekee,” alisema.

Abiria huonyeshwa vipimo vyao vya joto kwenye skrini, na wanapofika kwenye meza ya uhamiaji, wanachoonyesha ni visa na paspoti pekee.

“Wakati huu ambapo uchumi, shule na mipaka imefunguliwa, Afrika inahitaji mbinu madhubuti ya kupunguza hatari ya maambukizi ya corona. Ndio maana tumezindua teknolojia hii kupunguza kuenea kwa virusi hivi mipakani,” akasema Amira Mohammed, Kamishna wa Masuala ya Kijamii katika Tume ya AU.

You can share this post!

Polisi watibua maandamano ya wafuasi wa Bobi Wine jijini...

Mikakati ya UhuRaila kutuliza mlima